Siasa

Sakaja, Nyoro na Kiunjuri walengwa wakiambiwa wamkome Gachagua

June 1st, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

BAADHI ya wandani wa Naibu Rais Rigathi Gachagua wamewataka wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu), Mwangi Kiunjuri (Laikipia Mashariki) na Gavana wa Nairobi Bw Johnson Sakaja wakome dharau, hujuma na matusi kwa kinara huyo wao wa kisiasa.

Wakiongozwa na Mbunge wa Naivasha Bi Jayne Kihara, waliwataka watatu hao waelewe kwamba Bw Gachagua “alichangia pakubwa kuchaguliwa kwenu”.

“Viongozi hao watatu wamafaa kumheshimu Bw Gachagua kama kigogo wao,” akasema Bi Kihara.

Bw Sakaja tayari ashamkemea Bw Gachagua kama mnyanyasaji wa wadogo wake na ambapo amewaumiza kwa miaka miwili hadi sasa “lakini akitajwa wiki moja anaanza kulia huku akitorokea kwa msitu”.

Bw Gachagua alikiri kwamba kwa wiki nzima alikuwa ndani ya msitu wa Mlima Kenya akiwa amefunga kula na kunywa ili kuombea wenyeji wa Mlima Kenya wadumishe umoja na busara za kustahimili mipigo na misukosuko ya kisiasa.

Kwa upande wake, wandani wa Bw Nyoro wakiongozwa na Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu wamenukuliwa hadharani wakimtaka Rais William Ruto amutaliki Bw Gachagua kama mgombezi mwenza wake wa 2027 akisaka awamu ya pili usukani  na pia azimwe kuwa mrithi wa ikulu 2032.

Badala yake, wamependekeza kwamba Bw Nyoro ateuliwe kuwa mgombezi mwenza 2027 na mrithi wa ikulu 2032 wakimsema yeye ndiye mfaafu zaidi wa kuunganisha viongozi na wapiga kura wa Mlima Kenya.

Bw Kiunjuri naye tayari akiwa katika mahojiano na kituo cha runinga cha Inooro amemsuta Bw Gachagua kama wa kutenganisha Mlima Kenya kutokana na siasa za dharau, matusi na mabavu.

“Yeye anakimbia na kurandaranda Mlimani akiandamana na viongozi walio nyadhifani na pia nje akitukanana na pia kuwadunisha machoni mwa umma kisha analia kwamba kuna watu wa kutenganisha ilhali yeye ndiye mshukiwa mkuu,” akasema Bw Kiunjuri.

Aidha, Bw Kiunjuri alikuwa amenukuliwa akimtaka Bw Gachagua ajiondoe kwa serikali ya Rais William Ruto “na aende akaunde yake na hao anaoandamana nao”.

Bi Kihara alilalamika kwamba Bw Gachagua alitumia rasilimali zake na pia nguvu na ujuzi ndipo Rais Ruto akafanikiwa kulipenya eneo la Mlima Kenya na kisha kutawazwa mshindi wa urais.

Alikuwa akiongea mjini Limuru wakati msafara wa Bw Gachagua ulipitia hapo na kusimama kuhutubia wenyeji.

“Ikiwa Rais Ruto hakushinda vita vya ina maana kwamba wote watatu hao pamoja na sisi kwa saa hii tungekuwa hatuna mamlaka yoyote tukigugunwa na kijibaridi cha kuwa ndani ya upinzani,” akasema Bi Kihara.

Alisema ni aibu kubwa kuwaona na kuwasikiliza watatu hao wakimkosea Bw Gachagua heshima zake kama aliyewabeba kwa mabega, mgongo na kwa mapaja hadi kwa nyadhifa zao na kwa sasa wamejihisi watoshelevu zaidi kiasi cha kuwageuza kuwa wengi wa kiburi na ujeuri wa kimaongezi.

Mwanasiasa wa Laikipia Bi Cate Waruguru alimtaka Bw Kiunjuri aelewe kwamba “wewe sio wa ligi ya kiwango cha Bw Gachagua kwa kuwa hata hujawahi kupendekezwa kuwa Naibu Gavana…wewe ni mbunge tu Gachagua akiwa Naibu Rais”.

Alisema Bw Kiunjuri alipewa kazi ya ubunge Laikipia Mashariki kwa awamu ya nne sasa.

“Mbona hajawahi kujinyanyua kuwa na wadhifa wa juu kuliko ubunge?” akauliza Bi Waruguru.

Alimtaja Bw Gachagua kama jasiri ambaye hata hakuwa amemaliza awamu yake ya kwanza kama mbunge wa Mathira kabla ya kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa urais na kisha akafanikiwa kuwa Naibu Rais.

Bi Waruguru alimtaka Bw Kiunjuri atulie asomeshwe jinsi ya kung’aa kwa muda mfupi iwezekanavyo badala ya kuwa na haraka ya kujiangamiza kupitia tamaa ya kuongozwa na majivuno.

Mbunge wa Kajiado Kaskazini Bw Onesmus Ngogoyo aliteta kwamba “hawa watundu wetu wa kisiasa ni wasaliti tu wa kawaida ambao kile kinachowasumbua ni joto kwa misuli kutokana na minofu ambayo Bw Gachagua aliwasaidia kuangukia katika serikali”.

Alimtaka Bw Sakaja aelewe kwamba “wazee kutuliko ni wa kuheshimiwa”.

“Ikiwa kwenu hukupewa ushauri huo, malimwengu yatakufunza na 2027 tuko na wewe bampa kwa bampa Nairobi tukilenga kukupa adabu za kukutimua,” akasema Bw Ngogoyo.

Lakini mapema wiki hii Bw Sakaja alisema kwamba huo wadhifa wa ugavana sio wa kupeanwa bali huwa ni wa kupigiwa kura.

“Hata kama huwezi kuheshimu viongozi waliochaguliwa, basi heshimu wapigakura waliowachagua,” akasema Bw Sakaja.

Mbunge wa Embakasi Kaskazini Bw James Gakuya alisema kwamba “tutaonana na Sakaja Nairobi 2027″.

“Atulie tu na afurahie muda ambao amebaki nao kwa sasa kwa kuwa kwa uhakika siku ya kiama yaja na hatutambeba kwa migongo yetu tena sawa na jinsi tulivyofanya na Bw Gachagua katika uchaguzi mkuu wa 2022,” akasema Bw Gakuya.

Aliongeza kwamba wote ambao wamejipa mawazo butu kwamba wataweza kumwinda Bw Gachagua kumwangusha katika eneo la Mlima Kenya waelewe kwamba hilo haliwezekani na mapambano tayari yameanza.