Habari MsetoSiasa

Sakaja sasa amezea mate kiti cha Sonko

December 16th, 2019 3 min read

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Nairobi Johnston Sakaja amefichua kuwa yu tayari kuwania wadhifa wa ugavana wa Nairobi endapo Gavana Mike Sonko anayekabiliwa na kesi ya ufisadi atalazimishwa kuondoka afisini kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Hata hivyo, seneta huyo alifafanua kuwa ataendelea kuwahudumia wakati wa Nairobi kama seneta hadi 2022 endapo kiti hicho cha Sonko hakitatangazwa kuwa wazi kabla ya wakati huo.

“Ikiwa kiti cha ugavana kitasalia wazi na watu wa Nairobi waamue niwanie kiti hicho, basi nitawania. Ikumbukwe kuwa ni haki yangu ya kikatiba kuwania kiti hicho ikiwa watu wa Nairobi watahisi kuwa ninaweza kuwahudumia vizuri kama gavana,” Bw Sakaja akasema Jumapili usiku kwenye mahojiano katika kipindi cha “Punchline” kwenye runinga ya K24.

“Hata hivyo, ikiwa mzozo wa uongozi katika serikali ya Nairobi utasuluhishwa basi nitaendelea kuhudumu kama seneta wa Nairobi kwa miaka iliyosalia hadi nikamilishe muhula wangu wa miaka mitano,” Bw Sakaja akafafanua.

Wiki jana, Bw Sonko pamoja na maafisa wengine 12 wa kaunti ya Nairobi walishtakiwa kwa makosa mbalimbali ikiwa kupanga njama ya kutenda uhalifu wa kiuchumi, kufeli kuzingatia sheria ya utoaji zabuni hali iliyopelekea kampuni kadha kulipwa Sh357 milioni, pesa za umma, kinyume cha sheria.

Bw Sonko, na wenzake walioachiliwa kwa dhamana ya Sh15 milioni kila mmoja na mdhamini wa Sh30 milioni. Lakini Hakimu Mkuu wa Mahakama Kuu ya kupambana na ufisadi Dauglas Ogoti aliamuru kwa Bw Sonko na wenzake wasiingia katika afisi zai hadi kesi inayowakabiliwa itakaposikizwa na kuamuliwa.

“Wanaweza tu kuingia afisini mwaka kuchukua mali yao ikiwa wataandamana na maafisa wa upelelezi au mtu yeyote aliyepewa idhini,” akaongeza Bw Ogoti.

Uamuzi huo wa mahakama umeutumbukiza uongozi wa kaunti ya Nairobi katika mzozo wa uongozi kwa sababu kaunti imesalia bila gavana tangu Polycarp Igathe alipojiuzulu miezi 18 iliyopita. Tangu wakati huo Bw Sonko hajateua naibu gavana mpya.

Jaribio lake la kumpendekeza mwanaharakati wa mapinduzi Miguna Miguna lilitakaliwa mwaka jana na Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi na madiwani wa mrengo wa Jubilee wakidai wakili Miguna sio mwanachama wa chama hicho. Vile vile, walisema utata kuhusu uraia wake bado halijasuluhishwa.

Lakini licha ya kuzimwa kuingia afisini mwake, Sonko bado anashikilia kuwa bado ndiye anasimamia shughuli za serikali ya kaunti ya Nairobi akipinga dhana kwamba kuna ombwe la uongozi katika serikali hiyo.

Jumapili, Bw Sakaja alisema kuwa awali alikuwa akitaka kuwania kiti cha ugavana wa Nairobi katika uchaguzi mkuu wa 2017,”lakini nikabadili azma hiyo dakika za mwisho kulingana na hali ya kisiasa katika kaunti ya Nairobi wakati huo.”

Wiki jana Seneta Sakaja alimwandikia barua Spika wa Seneti Kennth Lusaka akimtaka aitishe kikao cha maalum cha bunge la Seneti ili maseneta wajadili hali ya uongozi katika kaunti ya Nairobi.

Anashikilia kuwa katika hali ya sasa ambapo Gavana amezuiwa kuingia afisini na hamna naibu gavana kushikilia wajukumu yake, kuna pengo ya uongozi katika serikali ya kaunti ya Nairobi ambayo inaweza kuchangia kuandaliwa kwa uchaguzi mdogo.

Hata hivyo, kikatiba, uchaguzi huo mdogo unaweza kufanyika tu ikiwa madiwani watamwondoa Sonko afisini kwa mujibu wa kipengele cha 181 (1) (a) (b) ili kuwe na pengo katika afisini ya gavana.

Vile vile, uchaguzi mdogo unaweza kufanyika ikiwa Rais Uhuru Kenyatta atatumia mamlaka aliyopewa na Kipengee cha 192 (1) (a) (b) na kuvunjilia mbali serikali ya kaunti ya Nairobi.

Kulingana na kipengele hicho, Rais anaweza kuchukua hatua kama hiyo ikiwa kuna mzozo mkali katika kaunti husika, au katika hali maalum kama endapo huduma katika Kaunti ya Nairobi zitakwama.

Hata hivyo, Sakaja anasema hana matumaini na mchakato wa kumwondoa mamlakani Sonko akitoa mfano wa Gavana wa Embu Martin Wambora ambaye aliondolewa mamlakani mara mbili na madiwani wa kaunti hiyo lakini akarejeshwa mamlakani na mahakama.

Sakaja pia anaonekana kutounga mkono wazo ya kuweka usimamizi wa serikali ya kaunti ya Nairobi chini ya bodi maalum, endapo Rais atavunja serikali hiyo kwa mujibu wa kipengee cha 192 cha Katiba.

Seneta huyo alisema hayo huku macho yote yakielekezwa kwa Rais Kenyatta na madiwani ya kaunti hiyo ambao ndio wanaweza kuamua hatima ya kaunti ya Nairobi wakati huu, ili kuzuia mzozo ambao huenda ukatokea.

Kwa mfano, katika hali ya sasa hakuna afisa ambaye anaweza kutia saini miswada itakayopitishwa na Bunge la Kaunti ya Nairobi kwa sababu hamna gavana na naibu wake.

Vile vile, hamna anayeweza kufanya uteuzi kwa nyadhifa mbalimbali katika baraza la mawaziri na idara zingine za serikali ya kaunti ya Nairobi ikizingatiwa kuwa baadhi ya maafisa wanashikilia nyadhifa hizo kama kaimu.