Habari Mseto

Sakaja uko wapi, walia wafanyabiashara Muthurwa taka zikirundikana


WAFANYABIASHARA katika soko la Muthurwa Kaunti ya Nairobi wamelalamikia rundo la taka ambalo ni hatari kwa afya wakiendelea na shughuli zao za kawaida.

Mwenyekiti wa soko hilo, Bw Nelson Githaiga Waithaka alisema rundo hilo la taka limekuwa likiongezeka kwa muda wa wiki moja. Sasa ameitaka kaunti iharakishe kuzoa taka hizo ili kuwaondolea hatari ya mkurupuko wa maradhi.

Pia amemtaka Mbunge wa Starehe, Bw Amos Mwago na Diwani wa wadi hiyo, Bw Mwaniki Kwenya kuingilia suala hilo na kuwaokoa wafanyabiashara.

“Wanasiasa hawa wanastahili kumleta Bw Sakaja hapa aone jinsi hali ilivyo. Ni hatari sana kuendeleza biashara huku rundo hili la taka likiwa hapa,” akasema Bw Waithaka kwa niaba ya wafanyabiashara 2,000.

Mmoja wa wachuuzi wa matunda aliambia Taifa Leo kuwa anakadiria hasara kwa kuwa taka zimeziba njia inayotumiwa na wateja kufikia kibanda chake.

“Hakuna mteja anayekuja kununua bidhaa hapa kwa sababu hawezi kupitia pale kutokana na harufu mbaya inayotoka kwenye takataka,” akasema mwanamke huyo, 38.

Si mara ya kwanza suala la takataka katika soko la Muthurwa linawatatiza wafanyabiashara. Mwezi uliopita, kaunti ililazimika kuondoa mlima wa takataka baada ya wafanyabiashara kulalamika na suala hilo kuangaziwa na vyombo vya habari.