HabariMakala

Sakata mpya ya mahindi serikalini yawaletea wakulima hasara kubwa

March 14th, 2018 3 min read

Na WAANDISHI WETU

Kwa ufupi:

  • Sehemu ya Sh7.1 bilioni zilizotengwa kwenye bajeti ya 2017/2018 kununua mahindi kutoka kwa wakulima nchini ilitumiwa kuwalipa wafanyabiashara wa kibinafsi 
  • Mgogoro uliopo sasa ulianza kampuni za kibinafsi zilipoagiza mahindi na kuyauzia Serikali, hatua ambayo imewaacha wakulima wa Kenya wakishikilia kiasi kikubwa cha mazao bila wa kuwanunulia
  • Kiunjuri asema kuwa wizara yake itaunda sheria katika kipindi cha miezi sita ijayo ili kuzimba mianya iliyosababisha hali ya sasa
  • Serikali iliwachezea shere wakulima wa mahindi kwa kuwa ilitumia pesa zilizotengewa wakulima kufadhili wafanyabiashara

NGUZO ya Rais Uhuru Kenyatta ya kuhakikisha Kenya imejitosheleza kwa chakula imeanza kukumbwa na changamoto kufuatia kushindwa kwa Wizara ya Kilimo kununua mahindi yaliyozalishwa na wakulima wa Kenya, na badala yake kukimbilia kuagiza kutoka Uganda.

Matokeo yake yamekuwa ni mabohari ya Bodi ya Nafaka (NCPB) katika North Rift kujaa mahindi kutoka Uganda, hivyo hakuna nafasi ya kuweka mahindi ya wakulima wa Kenya.

Pia sehemu ya Sh7.1 bilioni zilizotengwa kwenye bajeti ya 2017/2018 kununua mahindi kutoka kwa wakulima nchini ilitumiwa kuwalipa wafanyabiashara wa kibinafsi walioagiza mahindi kutoka Uganda mwezi Januari, hivyo Wizara ya Kilimo haina fedha za kununua mahindi yote yaliyovunwa na Wakenya.

Hali inatarajiwa kuzorota zaidi kutokana na mpango wa Kenya kununua magunia 6.6 milioni zaidi kutoka Uganda.

Matokeo yake yamekuwa ni kiasi kikubwa cha mahindi ya wakulima wa Kenya kutonunuliwa, hali ambayo imewanyima pesa za kununua mbegu na mbolea pamoja na kutayarisha mashamba kwa upanzi msimu huu.

Pia kuna hatari ya mahindi hayo kuoza kutokana na unyevu unaotokana na mvua inayoendelea kunyesha.

Wakulima katika maeneo ya Eldoret na Moi’s Bridge wamekuwa wakishauriwa na NCPB kupeleka mahindi katika mabohari ya Kisumu, Nakuru na Kakamega, jambo ambalo wanasema linawaletea hasara kubwa za uchukuzi.

“Tunashangaa kwa nini Serikali imekuwa ikituhimiza kuzalisha mahindi kwa wingi lakini sasa hainunui mazao yetu,” akasema Christopher Kiptum ambaye ni mkulima eneo la Moiben, Kaunti ya Uasin Gishu.

Msemaji wa NCPB, Titus Maiyo alieleza Taifa Leo kuwa wanafanya juhudi za kuhamisha mahindi kutoka mabohari ya North Rift hadi maeneo mengine ili kuwe na nafasi ya kuchukua mahindi zaidi kutoka kwa wakulima.

 

Wiki tatu

Lakini ilijitokeza Jumanne hilo huenda lisifanyike baada wakulima ambao wamesubiri kwa hadi wiki tatu katika mabohari ya NCPB mjini Nakuru kujulishwa kuwa bodi haitachukua mahindi zaidi kutoka kwao.

“Mnajulishwa kuwa ununuzi wa mahindi umesimamishwa mara moja,” ilisema notisi hiyo.

Baadhi ya wakulima walioathiriwa na hatua hiyo  walikuwa wametumwa kutoka Eldoret kupeleka mahindi yao Nakuru. Mmoja wao, Richard Telgut alisema yeye na wenzake 50 walishauriwa kupeleka mahindi yao Nakuru na wamekuwa huko kwa wiki tatu.

“Tulitumwa hapa na kuna wenzetu walioambiwa wapeleke Kisumu. Hii ni hasara tupu. Tumekodisha malori na tumekaa hapa muda huo wote. Hatimaye tumeambiwa tuondoke bila kununuliwa mahindi yetu,” akasema Bw Telgut.

Meneja wa NCPB tawi la Nakuru, Bw Alfred Korir alisema agizo hilo lilitoka makao makuu.

Mgogoro uliopo sasa ulianza kampuni za kibinafsi zilipoagiza mahindi na kuyauzia Serikali, hatua ambayo imewaacha wakulima wa Kenya wakishikilia kiasi kikubwa cha mazao bila wa kuwanunulia.

Malori yakisafirisha mahindi hadi bohari la Eldoret. Waziri wa Kilimo, Bw Mwangi Kiunjuri alikiri kuna pesa zilizotengwa kununua mahindi kutoka kwa wakulima wa Kenya ambazo zilitumiwa kulipia mahindi yaliyoagizwa kutoka Uganda. Picha/ Maktaba

Kufaidi kampuni

Kulingana na Mwenyekiti wa Muungano wa Wakulima (KFAPA), Bw Stanley Nduati, maafisa wa Serikali walioidhinisha kampuni za kibinafsi kuagiza mahindi kutoka Uganda walikuwa na nia ya kufaidi kampuni hizo kwa kuwa walijua vyema mahindi yaliyopelekwa katika mabohari ya NCPB na kulipiwa hayakuwa mavuno ya wakulima wa Kenya.

“Kile Serikali ilifanya ni kukiuka bajeti yake ya 2017/2018 iliyokuwa imetengewa pesa za kununua mahindi kutoka kwa wakulima wa hapa nchini. Waliolipa waagizaji hao wanafaa waelezee ni kwa msingi gani walitumia pesa za umma kufadhili wafanyabiashara wa sekta ya kibinafsi,” akasema Bw Nduati.

Bw Nduati anashangaa ni kwa nini Wizara ikaagiza mahindi ya nje ikizingatiwa kuwa wakulima wa Kenya walikuwa tayari wamevuna mahindi yao mwezi Novemba na Desemba.

Bw Nduati aliambia Taifa Leo kuwa waagizaji hao walikuwa wakinunua gunia la kilo 90 kutoka Uganda kwa Sh1, 800 na kuuzia serikali kwa Sh3, 200. Bei hiyo ya chini nchini Uganda pia inazua maswali ya sababu ya gharama za juu za kuzalisha mahindi nchini licha ya mpango wa mbegu na mbolea ya bei nafuu kwa wakulima.

Wafanyakazi wakipima uzani wa mahindi katika mojawapo ya mabohari ya nafaka nchini. Kwa mujibu wa mkurugenzi wa Muungano wa Wakulima wa Kenya (KFA), Kipkorir Menjo, serikali iliwachezea shere wakulima wa mahindi kwa kuwa ilitumia pesa zilizotengewa wakulima kufadhili wafanyabiashara. Picha/ Maktaba

Kiunjuri akiri

Waziri wa Kilimo, Bw Mwangi Kiunjuri alikiri kuna pesa zilizotengwa kununua mahindi kutoka kwa wakulima wa Kenya ambazo zilitumiwa kulipia mahindi yaliyoagizwa kutoka Uganda.

“Serikali ilikuwa imepanga bajeti ya kununua magunia 2.4 milioni kutoka kwa wakulima lakini tumejipata katika hali ambapo serikali ilinunua magunia 3.4 milioni kutoka nje, huku kukiwa na mahindi mikononi mwa wakuzaji wetu.

Nikiangalia rekodi za wizara hii ambayo niliichukua tu hivi majuzi, ninaona kwamba maghala ya serikali yamejaa mahindi na hakuna pesa za kununua mahindi kutoka kwa wakulima wa hapa nchini ambao wanakadiriwa kuwa na magunia 1.2 milioni ya ziada,” akaambia Taifa Leo.

Bw Kiunjuri alisema kuwa wizara yake itaunda sheria katika kipindi cha miezi sita ijayo ili kuzimba mianya iliyosababisha hali ya sasa.

Alisema kuwa ataomba ufadhili wa ziada katika bajeti ndogo ili apate pesa za kununua mahindi kutoka kwa wakulima, huku ile ambayo iko katika maghala ya serikali ikipeanwa kwa wahanga 3.4 milioni wanaokumbwa na makali ya njaa kwa sasa.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa Muungano wa Wakulima wa Kenya (KFA), Kipkorir Menjo, serikali iliwachezea shere wakulima wa mahindi kwa kuwa ilitumia pesa zilizotengewa wakulima kufadhili wafanyabiashara.

Anasema kuwa hata ikiwa kuna mkataba wa kimaelewano kuhusu biashara kati ya Kenya na Uganda, mahindi hayo yangehusisha biashara ya kibinafsi bali sio kuuziwa Serikali.

 

Ripoti za BARNABAS BII, MAGDALENE WANJA Na MWANGI MUIRURI