HabariSiasa

SAKATA YA DHAHABU: Haji aonya wanaosambaza rekodi ya sauti mitandaoni

May 19th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji ameamuru Inspekta Jenerali wa Polisi Hilary Mutyambai kuhakikisha kuwa uchunguzi unaendelea kuhusu sakata ya dhahabu feki umekamilishwa na faili ya uchunguzi kuwalisishwa kwake ndani ya muda wa siku saba.

Aliahidi kuchukua hatua za kisheria kwa washukiwa pindi atakapopokea faili hiyo.

Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari, Bw Haji pia alionya umma dhidi ya kusambaza, kupitia mtandao wa kijamii, rekodi ya mawasiliano kati ya watu wawili kuhusiana na sakata hiyo inayochunguzwa kuhusu dhahabu feki kupatikana jijini Nairobi.

“Hisia zangu zimevutiwa na kanda ya sauti inayozungushwa mitandaoni ambapo madai yanayotolewa na watu wawili wanaozungumza kuashiria kuwa habari fulani ziliwasilishwa kwa Rais, aliyekuwa Waziri Mkuu na Waziri Matiang’i,” akasema.

“Madai kama hayo, na kusambazwa kwayo kupitia mitandao ya kijamii, hayafai kwa sababu yanaweza kuzua taharuki bila sababu yoyote,” Bw Haji akaongeza.

DPP alisema hadi pale ukweli wote utapatikana na kuchambuliwa, ni makosa kusambaza rekodi za mawasiliano kama hizo kwa umma.

Bw Haji alisema yeye binafsi amepokea malalamishi kutoka kwa wahasiriwa wa sakata wakidai kuwa watu waliotajwa wamekuwa wakiwasiliana nao kwa muda sasa huku wakitaja jina la Rais katika shughuli zao na mawasiliano.

“Baada ya kugundua kuwa walihadaiwa kuhusu uwepo wa dhahabu na madai ya uwongo kwamba Rais, aliyekuwa Waziri Mkuu na Waziri Matiang’i walifahamu kuhusu shughuli hizo, waliamua kutoa ripoti kwa maafisa wa Kenya. Pia waliamua kushirikiana na walinda usalama kufichua ukweli kuhusu shughuli hizo,” akasema Bw Haji.

DPP alitoa wito kwa Wakenya ambao wanaweza kuwa na habari kuhusu sakata hizo kutoa ripoti wa asasi za usalama, ili kulinda hadhi ya uchunguzi unaoendelea sawa na ushahidi na mashahidi.

“Lengo la uchunguzi wowote wa kitendo cha uhalifu ni kuhakikisha washukiwa wanawajibika. Hii inaweza tu kufanyika wakati ambapo uchunguzi unaendeshwa katika mazingira tulivu, pasina uvumi na vitisho. Kwa sababu hiyo, naomba kila mmoja aliye na habari ambazo zinaweza kusaidia katika uchunguzi unaoendelea kuziwasilisha kwa asasi zinazoendeshaa uchunguzi,” Bw Haji akasema.