Habari Mseto

Sakata ya Kenya Power yaudhi Benki ya Dunia

October 3rd, 2018 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

KASHFA ya uteuzi wa kampuni za kutoa huduma za uchukuzi na uwekezaji kwa Kenya Power (KP) imeudhi Benki ya Dunia (WB), mashirika ya kutoa misaada ya kimataifa, Bunge la Seneti na Kitaifa, mahakama inayosikiza kesi za ufisadi ilifahamishwa Jumatano.

Meneja mkuu wa ukaguzi wa KP Bw Charles Cheruiyot Kipng’eno alisema kampuni nyingi ambazo hazikuwa zimewasilisha maombi ya kutoa huduma za uchukuzi na uwekezaji (L&T) ziliteuliwa.

Bw Kipng’eno alisema kuwa kampuni hizo ziliorodheshwa baada ya ufunguzi wa zabuni na wanachama wawili wa kamati hiyo Bw Bernard Githui Muturi na Mhandisi Evelyne Pauline Amondi.

Bw Kipng’eno alisema kashfa hiyo iliporipotiwa na kuchapishwa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, “Maafisa wa Benki ya Dunia , Wanakamati wa kamati za kawi za Mabunge ya Seneti na Bunge la kitaifa na maafisa 10 kutoka kwa idara ya uchunguzi wa jina (DCI) walienda afisini mwake kupewa nakala ya ripoti ya uchunguzi wa kashfa hiyo aliyotayarisha.”

Meneja huyo alisema zabuni hiyo haikupasa kufunguliwa na wanachama wawili kama ilivyofanywa na Bw Muturi na Bi Amondi.

Mwanachama wa tatu wa kamati hiyo Bw David Makenzi aliyekuwa ameteuliwa na Mkurugenzi mkuu wa KP Dkt Ken Tarus hakufika wakati wa ufungunzi wa zabuni hiyo.

“Kwa vile Dkt Tarus alikuwa afisini, wanachama wa kamati ya zabuni na ukaguzi hawakupasa kuifungua baada ya Bw Makenzi kukosas kufika kushiriki katika hafla hiyo,” alisema Bw Kipng’eno.

Mkaguzi wa Kenya Power Charles Kipng’eno akitoa ushahidi mahakamani Oktoba 3, 2018. Picha/Richard Munguti

Meneja huyo ambaye ushahidi wake uliungwa mkono na mkaguzi na mchunguzi wa KP Bw Argwings Kodhek Ochily alisema “kile kingelifaa  ni ufunguzi wa zabuni hiyo kufutiliwa mbali baada ya Bw Makenzi kutofika.”

Mabw Kipng’eno na Ochily walimweleza hakimu mkuu Bw Lawrence Mugambi kwamba sheria za zabuni  husema, “ikiwa mwanachama mmoja kati ya hao watatu hajafika basi zoezi lote lapasa kufutiliwa mbali.”

Wawili hao walikuwa wanatoa ushahidi katika kesi ambapo Dkt Tarus na wahandisi wanane wakuu waliohusika na utoaji zabuni hiyo.

Walioshtakiwa ni Dkt Tarus, wahandisi Harun Karisa, Daniel Tare, Noah Ogano O Omondi, Daniel Ochieng Muga, John Mwaura Njehia, James Muriuki, Bw Muturi na Bi Amondi.

Wote tisa wanakabiliwa na shtaka la kuidhinisha makampuni ambayo hayakuwa yamehitimu kutoa huduma za L&T na kupelekea KP kupoteza zaidi ya Sh159 milioni.

Wamekana waliidhinisha kampuni hizo kati ya  Aprili 12, 2017 na Juni 12, 2018.

Mahakama iliambiwa kufunguliwa kwa tenda hiyo na wanachama wawili Bw Muturi na Mhandisi Amondi kulikaidi sheria nambari 78(1)(a) ya sheria za ufunguzi wa zabuni.

Kesi inaendelea.