HabariSiasa

SAKATA YA MABWAWA: Mbadi awataka Ruto na Murkomen kujiuzulu

July 22nd, 2019 2 min read

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Wachache katika Bunge la Kitaifa John Mbadi sasa anamtaka Naibu Rais William Ruto kujiuzulu mara moja kufuatia tuhuma zinazomkabili Waziri wa Fedha Henry Rotich kuhusiana na sakata ya mabwawa ya Arror na Kimwarer.

Bw Mbadi ambaye pia ndiye mwenyekiti wa chama cha ODM pia alimtaka kiongozi wa wengi katika bunge la seneti Kipchumba Murkomen kujiuzulu kwa kudai kuwa hakuna pesa zililizopotea katika sakata hiyo.

“Naibu Rais Ruto na wandani wake kama vile Kipchumba Murkomen walijitokeza waziwazi kudai kuwa hakuna makosa yalitenda na kwamba hamna pesa zilipotea katika sakata hii. Sasa imebainika kuwa madai yao hayakuwa na ukweli wowote na hivyo wanapaswa kujiuzulu kwa kuonekana kulinda wezi wa pesa za umma,” akasema Bw Mbadi Jumatatu.

Mbunge huyo wa Suba Kusini pia alimtaka Dkt Ruto na Bw Murkomen kuwaomba msamaha Wakenya kwa kuwapotosha kuhusiana na sakata hiyo ambapo takriban Sh21 bilioni zinadaiwa kupotea au kulipwa kinyume cha sheria.

Itakumbukwa kwamba mnamo Aprili mwaka huu Naibu Rais alipuuzilia mbali madai ya Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti kwamba jumla ya Sh21 bilioni zilipotea katika sakata hiyo.

Akiongea katika majengo ya Mahakama ya Juu mbele ya bosi wake, Rais Uhuru Kenyatta Dkt Ruto alidai kuwa ni hitilafu ya Sh7 bilioni pekee ilitokea katika malipo ya awali ya ujenzi wa mabwawa hayo.

“DCI anawahadaa Wakenya kwa madai ya uwongo kwamba jumla ya Sh21 bilioni zilipotea katika kile ambacho anadai kuwa sakata ya ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer. Kwanza, hakuna sakata hapa. Pili, hitilafu ambayo ilitokea na ya malipo ya Sh7 bilioni ambayo inalindwa na udhamini wa benki uliowekwa na mwanakandarasi,” akasema Dkt Ruto.

Hata hivyo, Rais Kenyatta alikubaliana na kauli ya Bw Kinoti na kumhimiza kuendelea na uchunguzi kwa lengo la kuwanasa wahusika hali katika wizi wa pesa hizo.

Kwa upande wake Bw Murkomen alitumia majukwaa mbalimbali kama vile mikutano ya hadhara katika maeneo kadhaa ya Rift Valley kumkashifu Bw Kinoti akisema afisi anatumiwa na maadui wa kisiasa wa Dkt Ruto kuzima azma yake (Ruto) ya kuwania urais 2022.

Waziri wa Fedha Bw Henry Rotich na maafisa wengine wa serikali ambao walikamatwa Jumatatu watafikishwa Mahakamani Jumanne kwa tuhuma za kuhusika katika sakata ya wizi wa Sh21 bilioni za ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer watasimamishwa kazi.

Hii ni kufuatia agizo ambalo lilitolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji akisema afisi yake imepokea ushahidi wa kutosha kuwashtaki washukiwa hao.

Watashtakiwa kwa makosa ya matumizi mabaya ya afisa, njama ya kutekeleza udanganyifu kinyume cha sheria, kuanza utekelezaji wa mradi bila kufanya maandalizi hitaji, kutozingatia sheria ya usimamizi wa fedha za umma na ukiukaji wa Sheria kuhusu Utoaji zabuni kwa kuipa zabuni kampuni ya CMC di Ravenna kutoka Italia.

Kampuni hiyo ndio ilipewa zabuni ya ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer katika kaunti ya Elgeyo Marakwet wenye thamani ya Sh63 bilioni.

Bw Haji aliongeza kuwa Rotich na wenzake sharti wajiondoe afisini baada ya kujibu mashtaka kadhaa yanayowakabili.

“Sharti waondoke afisini kwa muda… hawa sio magavana. Nitamwandikia Mkuu wa Utumishi wa Umma. Nitafanya hivyo sasa hizi. Hii ndio sheria. Ikiwa umeshtakiwa na ukajibu mashtaka, lazima ukae kando kwa muda kutoa nafasi kukamilishwa kwa kesi dhidi yako,” Bw Haji akawaambia wanahabari alipoulizwa ikiwa itabidi washukiwa hao kuondoka afisini.