Habari Mseto

SAKATA YA NYS: Benki sita kuchunguzwa zilivyosaidia wizi wa mabilioni

May 29th, 2018 2 min read

Na BENSON MATHEKA

UCHUNGUZI wa kashfa za mabilioni ya pesa kutoka idara za serikali sasa utaelekezwa katika benki ambazo pesa hizo zilipitishwa, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji amesema.

Akihutubia wanahabari jijini Nairobi Jumatatu, Bw Haji alihakikishia Wakenya kwamba uchunguzi utakuwa wa kina.

Wakenya wanasema kwamba kiwango cha pesa zilizohusika ni kikubwa na sheria ya ulanguzi wa pesa lazima ilikiukwa na benki husika.

Kulingana na wapelelezi, benki sita zilihusika katika sakata ya Shirika la Taifa la Huduma kwa Vijana (NYS).

Maswali pia yameulizwa kuhusu uwajibikaji wa Benki Kuu ya Kenya (CBK) na shirika la serikali la kuripoti masuala ya fedha yanayotiliwa shaka (FRC) hasa baada ya ripoti za uchunguzi kubaini kwamba baadhi ya malipo yalikuwa yakiidhinishwa mara moja kutoka mfumo wa pamoja wa kutoa pesa wa serikali (IFMIS).

Kulingana na ripoti, baadhi ya malipo yalikuwa yakiidhinishwa saa moja baada ya mwenye akaunti kutaka kutoa pesa. Sheria ya kukabiliana na ulanguzi wa pesa inasema benki zinapaswa kuripoti visa vyovyote vya huduma zisokuwa za kawaida kwa CBK na FRC. Ikiwa benki zilizohusika ziliripoti shughuli hizo, mashirika hayo yatalizimika kueleza hatua yalizochukua.

Gavana wa CBK Patrick Njoroge (pichani) na mkuu wa FRC Saitoti Kimerei Maika wataeleza hayo watakapofika mbele kamati ya uhasibu ya bunge ambayo iliahidi kuwaita.

Kulingana na sheria ya kukabiliana na ulanguzi wa pesa ya 2009, FRC inafaa kupokea, kuchanganua na kutafsiri ripoti za shughuli za kutia shaka katika mfumo wa benki nchini Kenya.

Wadadisi wa masuala ya kifedha wanadai kwamba kuna sheria za kuwezesha benki kugundua malipo ya ufisadi lakini nyingi zinazipuuza.

Kanuni zilizotolewa kwa benki 2016 katika juhudi za kukabiliana na ulanguzi wa pesa zinakataza utoaji wa zaidi ya Sh1 milioni bila kuidhinishwa na Benki Kuu.

Kanuni hizo zilitolewa kufuatia madai ya wizi wa mabilioni ya pesa kutoka NYS kupitia sakata ya kwanza iliyogharimu walipa ushuru Sh1.6 bilioni.

Chini ya kanuni hizo, mteja anafaa kujaza fomu ya lazima ya kutoa pesa akieleza anakotaka kuzipeleka na matumizi yake.

Aidha, anafaa kueleza kwa nini kiwango kikubwa cha pesa kinahitajika na kwa nini hawezi kutumia mfumo wa kielektroniki wa kuhamisha pesa.

Maswali mengine anayofaa kueleza ni pesa zilikotoka na wale wanaofaa kufaidika.