Habari Mseto

SAKATA YA NYS: Dhamana ya Lillian Omollo yakubaliwa,aondoka gerezani

June 22nd, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

KATIBU mkuu Wizara ya Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia Bi Lillian Omollo alikuwa wa kwanza kuruhusiwa kuondoka gerezani baada ya dhamana alizowasilisha kukubaliwa na mahakama.

Bi Omollo na washukiwa wengine wawili watapumua hewa safi wakiwa huru baada ya kukaa gerezani siku 26 tangu Mei 28, 2018 walipozuiliwa baada ya kushtakiwa kwa sakata ya NYS iliyopelekea zaidi ya Sh460milioni kupotea.

Bi Omollo ataondoka gereza la Langata anakozuiliwa baada kutupiliwa mbali kwa ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kwamba dhamana zote watakazowasilisha washtakiwa zikaguliwe na kuidhinishwa na shirika la urejeshaji mali ya umma iliyoibwa ARA.

Katika barua aliyokuwa ameandikia mahakama Alhamisi Bw Haji alikuwa ameitaka korti iruhusu ARA iidhinishe dhamana hizo  alizosema huenda zilinunuliwa na pesa zilizoibwa NYS.

Ombi hili lilipingwa vikali na mawakili wanaowatetea washtakiwa wakisema Bw Haji anajaribu kuhujumu maagizo ya korti.

Akitupilia mbali ombi hilo la Bw Haji hakimu mwandamizi Bw Lawrence Mugambi ni mahakama tu iliyo na mamlaka ya kukataa dhamana na kuruhusu zoezi la ukaguzi liendelee.

Bw Mugambi alisema DPP hana mamlaka kisheria kuweka masharti mapya katika utaratibu wa kuwahoji wadhamini na uhalali wa dhamana walizowasilishwa washtakiwa.

Alisema kuwa Bw Haji atakiuka sheria ikiwa ataruhusiwa kuvuruga maamuzi ya mahakama kuu iliyoweka masharti ya kuachiliwa kwa dhamana kwa washukiwa hao wa sakata ya NYS ambapo zaidi ya Sh400milioni zillibwa kwa kulipia huduma ambazo hazikutolewa.

Mahakama kuu iliwaachiliwa washtakiwa hao Juni 19 2018.

Akiwaachilia kwa dhamana Jaji Hedqig Ong’udi aliamuru kila mshukiwa awasilishe dhamana ya Sh5 milioni na mdhamini wa Sh2 milioni pamoja na dhamana ya pesa tasilimu Sh1milioni.

Bw Mugambi alisema suala alilozua DPP ni nzuri katika jitihada za kupambana na ufisadi lakini halikuwa moja ya masharti ya Jaji Ong’undi.

Alisema kama DPP angelitaka ARA ishirikishwe katika ukaguzi wa dhamana , angeliomba Jaji Ong’undi atoe agizo kwamba dhamana zote ziidhinishwe na shirika hili la urejeshaji mali ya umma iliyoibwa.

“Sitamruhusu DPP awe kizingiti katika utekelezaji wa maagizo ya Mahakama kuu katika ukaguzi wa dhamana na mahojino na wadhamini,” alisema Bw Mugambi.

Hakimu huyo alisema Jaji Ong’undi alikuwa ameamuru wadhamini wakaguliwe na mahakimu wa mahakama zinazosikiza na kuamua kesi za ufisadi.

Wakipinga masharti hayo mapya aliyowasilisha DPP, mawakili Dunstan Omari, Cliff Ombeta, Kirathe Wandugi walisema kinara huyu wa mashtaka anavuruga utenda kazi wa mahakama akiwa na nia “ washtakiwa wote 47 washindwe kulipa dhamana waliyopewa.”

Bw Omari aliomba korti imwekee muda Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI)  muda wa siku tatu au wiki moja akamilishe kukagua uhalali wa dhamana walizowasilisha washtakiwa na kutoa ripoti kwa mahakama.

“Tutakaa hapa muda wa miezi mitatu au minne na hata mwaka ikiwa Polisi na DPP wataruhusiwa kuvuruga utaratibu wa kuidhinisha dhamana zilizowasilishwa na washtakiwa hawa 47,” alisema wakili Assa Nyakundi.

Lakini mahakama iliamuru shughuli ya kukagua wadhamini iendelee na ikiwa kutaimbuka suali kuhusu dhamana yoyote ile basi DPP atakuwa huru kuapa Afidaviti akiomba ARA ichunguze dhamana husika.

“Kila mshtakiwa atakaguliwa kivyake. Ikiwa kutazuka swali kuhusu dhamana zitakazowasilishwa na washtakiwa basi DPP kupitia afisa anayechunguza kesi hiyo Bw Paul Waweru atahoji stakabadhi hiyo,” Bw Mugambi aliamuru.