Habari Mseto

SAKATA YA NYS: Kesi yaanza rasmi

November 1st, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

KESI ya kashfa ya Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) dhidi ya washtakiwa 37 iliyopelekea zaidi ya Sh11bilioni kupotea ilianza kusikizwa Jumatano.

Shahidi wa kwanza Bw Sebastian John Mokua alianza kutoa ushahididi dhidi ya aliyekuwa katibu mkuu Bi Beatrice Mbogo Omollo na aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa NYS Bw Richard Ndubai miongoni mwa wengine.

Bw Mokua aliambia mahakama kuwa makampuni 36 yalipeleka maombi ya kutoa huduma mbali mbali kwa NYS.

Katika ya huduma zilizopelekewa maombi ni uuzaji wa vyakula , makaratasi na bidhaa nyinginezo.

Bw Mokua alisema kuwa Bi Lucy Wambui Ngirita , mamayake Bi Anne Wambere Ngirita alikuwa amepewa zabuni ya kuuzia NYS vyakula katika kampi ya Gigiri.

Kutokana na mauzo hayo ya chakula , Lucy Njeri anashtakiwa alipokea ShSh63,254,008 kupitia kwa kampuni yake-Ngiwaco Enterprises.

Malipo hayo yaliidhinishwa na Bi Omollo.

Bw Mouko alisema kati ya makampuni hayo 36 ni manne tu yaliyoteuliwa.

Bw Mouko ni mmoja wa mashahidi 43 waliorekodi taarifa dhidi ya washtakiwa hao 37.

Jumatatu wiki hii washtakiwa hao walifunguliwa mashtaka mapya 82 ya matumizi mabaya ya mamlaka na kulipwa kwa huduma ambazo hazikutolewa

Katika kesi hiyo yenye mashtaka 82 , Bi Omollo , aliyekuwa mkurugenzi mkuu Bw Richard Ndubai na washukiwa wengine 28 akiwamo Bi Anne Wambere Ngirita wameshtakiwa kuifuja Serikali kupitia kwa NYS Sh226,945,258.

Bi Omollo amedaiwa alitumia mamlaka ya afisi yake vibaya kwa kuidhinisha malipo ya Sh54,848,750 kwa Bi Anne Wambere Ngirita kupitia kwa kampuni yake ijulikanayo kwa jina Annwaw Investment Limited.

Pia Bi Omollo ameshtakiwa kuidhinisha malipo ya Sh63,254,008 kwa Bi Lucy Wambui Ngirita kupitia kwa kampuni yake-Ngiwaco Enterprises.

Pia alimlipa By Phyilis Njeri Ngirita Sh50,970,500 kupitia kwa kampuni yake –Njewanga Enterprises.

Mbali na hao dada Bi Omollo alishtakiwa kwa kumlipa baba yao Bw Jeremiah Gichiri Ngirita Sh57,872,000 kupitia kwa kampuni yake-Jerrycathy Enterprises aliomiliki pamoja na mkewe (njeri).

Bw Ndubai , aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa NYS ameshtakiwa kwa kuidhinisha malipo ya Sh16, 590,000 kwa Bi Phyilis Njeri Ngirita kupitia kwa kampuni yake Njewanga.

Bi Anne Wambere Ngirita ameshtakiwa kwa kuifuja NYS Sh54,848,750 bila ya kutoa huduma zozote.

yake Anne, Bw Jeremiah Gichini Ngirita alikana alipokea Sh57,872,000 kutoka kwa NYS bila ya kutoa huduma zozote.

Lucy na mama yake Njeri Ngirita walikana walitia kibidoni zaidi ya Sh114m kutoka kwa NYS bila ya kutoa huduma zozote.

Washtakiwa walikanusha mashtaka mapya yaliyowasilishwa dhidi ya wafanyakazi hao wa zamani wa NYS na wafanya biashara hwa wa familia ya Ngirita.

Kesi inaendelea.