Habari MsetoSiasa

SAKATA YA NYS: Wabunge wa Jubilee na Nasa wataka Waziri Kariuki ang’atuliwe

June 7th, 2018 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE watano Alhamisi walimtaka Waziri wa Afya Bi Sicily Kariuki ajiuzulu la sivyo watamtimua afisini kuhusiana na sakata ya Sh9 bilioni katika Shirika la Huduma za Vijana kwa Taifa (NYS).

Wakiongozwa na Mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro wabunge hao kutoka mirengo ya Jubilee na NASA, pia walimtaka Rais Uhuru Kenyatta kumsimamisha kazi Bi Kariuki la sivyo waanzishe mchakato wa kumng’oa mamlakani kwa kupitisha hoja ya kutokuwa na imani naye bungeni.

Huku wakipendekeza kushtakiwa kwa waziri huyo, wabunge hao walidai kuwa washukiwa 43 waliokamatwa juzi, wakiwemo Katibu wa Wizara Lilian Omollo na Mkuregenzi wa NYS Richard Ndubai, “ni samaki wadogo”.

Pesa hizo zilipotea katika mwaka wa 2016, Bi Kariuki akiwa mamlakani kama waziri aliyesimamia NYS.

“Kitendawili cha sakata ya NYS hakiwezi kuteguliwa ikiwa Bi Sicily Kariuki hataondoka afisini kisha afunguliwe mashtaka. Haiwezekani kwamba Sh9 bilioni zinaweza kupotea au kuibiwa bila waziri kujua,” Bw Osoro, ambaye ni Mbunge wa chama cha Kenya National Congress (KNC), alisema jana kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge.

Aliandamana na wabunge Moses Kirima (Imenti ya Kati, Jubilee), Tindi Mwale (Butere, ANC), Abdikarim Osman (Fafi, Kanu) na Meja Bashir Abdulahi (Mandera Kaskazini, Jubilee).

Wabunge hao walisema wanamuunga mkono Rais Kenyatta pamoja na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga kutokana na kujitolea kwao kupambana na ufisadi, wakiahidi kupiga jeki mchakato huo kwa kupitisha sheria husika bungeni.

Washukiwa 43 wa sakata hiyo wangali kwenye rumande baada ya Hakimu Mkuu Douglas Ogoti kuwanyima dhamana.

Wito wa jana ni wa pili kutolewa na wabunge mwaka huu kumtaka Waziri Kariuki kuondoka afisini. Shinikizo za kwanza zilianzishwa Machi mwaka huu.

wabunge 170 walipotia saini hoja ya kumtaka ajiuzulu kwa kumsimamisha kazi aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) Bi Lily Koros.

Hoja hiyo ilifeli kuwasilishwa bungeni baada ya Rais Kenyatta na Naibu wake William Ruto kuingilia kati.