Michezo

Salah afunga mabao matatu na kuongoza Liverpool kupepeta Leeds United ligini

September 13th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

LEEDS United walirejea katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa mara ya kwanza baada ya miaka 16 kwa matao ya juu katika mechi iliyowashuhudia wakitikisa uthabiti wa Liverpool ugani Anfield mnamo Septemba 12, 2020.

Liverpool ambao walitawazwa mabingwa wa EPL kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 msimu uliopita, walioongoza mechi mara tatu huku Leeds ya kocha Marcelo Bielsa ikitoka nyuma kila mara na kusawazisha.

Ilikuwa penalti ya dakika ya mwisho kutoka kwa fowadi Mohamed Salah ndiyo iliyowezesha Liverpool kuwazamisha Leeds United kwa mabao 4-3 katika mechi hiyo ya ufunguzi wa msimu mpya wa 2020-21.

Penalti iliyofumwa wavuni na Salah ilitokana na tukio la sajili mpya wa Leeds, Rodrigo Moreno, kumchezea Fabinho visivyo katika dakika ya 88.

Salah aliyefunga mabao matatu katika mechi hiyo, alifungua ukurasa wa magoli kunako dakika ya nne kupitia penalti baada ya beki raia wa Ujerumani, Robin Koch kunawa mpira.

Hata hivyo, Leeds walisawazisha kupitia kwa Jack Harrison katika dakika ya 12 kabla ya masihara ya mabeki yao kumruhusu difenda Virgil van Dijk kurejesha Liverpool uongozini katika dakika ya 20.

Utepetevu wa Van Dijk katika dakika ya 30 uliwapa Leeds fursa ya kusawazisha kupitia kwa Patrick Bamford kabla ya Salah kukamilisha ufungaji katika kipindi cha kwanza dakika tatu baadaye.

Mechi hiyo ilishuhudia refa akikataa kuhesabu jumla ya mabao manne. Dalili zote ziliashiria kwamba Leeds wangaliondoka Anfield wakiwa na alama moja kapuni baada ya Mateusz Klich kufunga bao la kusawazisha katika dakika ya 66.

Liverpool waliendeleza rekodi yao ya kutoshindwa katika uwanja wao wa nyumbani katika jumla ya mechi 60 za EPL. Kufikia sasa, miamba hao wameibuka na ushindi katika mechi 49 na kuambulia sare mara 11.

Chelsea waliwahi kupiga jumla ya mechi 86 bila ya kushindwa katika uwanja wao wa Stamford Bridge kabla ya rekodi hiyo kukomeshwa mnamo Oktoba 2008. Awali, Liverpool walikuwa wamepiga jumla ya mechi 63 bila ya kushindwa hadi kufikia Disemba 1980.

Ilikuwa mara ya pili kwa mechi ya EPL kuchezewa katika siku ya kwanza ya msimu kushuhudia jumla ya mabao matano yakifungwa kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza. Manchester United waliwahi kupiga Fulham 5-1 mnamo Agosti 2006 huku Man-United wakiongoza kwa 4-1 kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza.

Ilikuwa pia mara ya kwanza kwa Liverpool kufungwa mabao matatu katika mechi ya ligi nyumbani tangu Septemba 1982.

Liverpool kwa sasa wameshinda kila mojawapo ya mechi zao 35 zilizopita ligini ambapo Salah amefunga. Raia huyo wa Misri amevunja rekodi ya Wayne Rooney aliyewahi kufunga jumla ya mabao 34 mfululizo katika mechi zilizoshuhudia Man-United wakiibuka washindi kati ya Septemba 2008 na Februari 2011.

Liverpool kwa sasa wana wiki nzima ya kujiandaa kwa gozi dhidi ya Chelsea mnamo Septemba 20, 2020 uwanjani Stamford Bridge huku Leeds wakitarajiwa kunogesha raundi ya pili ya Carabao Cup dhidi ya Hull City uwanjani Craven Cottage mnamo Septemba 16, 2020.