Salah afyeka tuzo zote EPL, sasa ashinda Bao Bora la Msimu

Salah afyeka tuzo zote EPL, sasa ashinda Bao Bora la Msimu

Na GEOFFREY ANENE

MOHAMMED Salah yumo mbioni kujiongezea taji la goli bora la msimu baada ya kupata asilimia 26 ya kura za mashabiki zilizoandaliwa na Shirika la Utangazaji la BBC.

Mwanaasoka huyu bora wa Afrika mwaka 2017 aliibuka mfungaji bora kwenye Ligi Kuu ya Uingereza kwa mabao 32 na pia mwanasoka bora wa msimu 2017-2018 nchini Uingereza.

Shughuli ya kupigia kura goli tamu la msimu ilikamilika Mei 13, 2018 saa tano na dakika 50 usiku, huku bao la mvamizi huyu matata wa Misri dhidi ya Tottenham hapo Februari 4, 2018 likiibuka mshindi.

Muingereza Jamie Vardy, ambaye ni mali ya Leicester, alikamilisha katika nafasi ya pili kwa asilimia 22 kutokana na bao lake dhidi ya West Brom mnamo Machi 1, 2018.

Mshambuliaji Muingereza Wayne Rooney alizoa asilimia 11 ya kura zilizopigwa kwa kufungia Everton bao tamu dhidi ya West Ham mnamo Novemba 29, 2017. Rooney alishinda goli bora la msimu mara tatu (msimu 2004-2005, 2006-2007 na 2010-2011) akichezea Manchester United.

Kiungo Mkenya Victor Wanyama aliambulia asilimia 10 baada ya kupachika bao safi kutoka nje ya kisanduku na kusaidia klabu yake ya Tottenham kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Liverpool uwanjani Anfield hapo Februari 4, 2018.

Mhispania Pedro Obiang, ambaye mizizi yake ni Equatorial Guinea, alivuna asilimia tisa ya kura zilizopigwa kwa kufungia West Ham bao dhidi ya Tottenham mnamo Januari 4, 2018 naye Mmoroko Sofiane Boufal kutoka klabu ya Southampton akapata asilimia nane kwa bao lake safi dhidi ya West Brom mnamo Oktoba 21, 2017.

Muingereza Charlie Daniels (Bournemouth) na Mjerumani Leroy Sane (Manchester City) waliambulia asilimia saba ya kura zilizopigwa kila mmoja kutokana na mabao yao dhidi ya Manchester City mnamo Agosti 26, 2017 na Arsenal hapo Machi 1, 2018, mtawalia.

You can share this post!

Levante yaiharibia Barcelona karamu ya kutoshindwa

ODM yajitosa kwa kashfa ya Sh9 bilioni NYS

adminleo