Michezo

Salah, Mane, Koulibaly, Benatia na Partey kuwania Mwanasoka Bora wa BBC

November 19th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

ORODHA ya wanasoka watakaowania tuzo ya Mwanasoka Bora wa BBC Barani Afrika mwaka wa 2018 imetangazwa.

Wawaniaji watakuwa Medhi Benatia (Morocco), Kalidou Koulibaly (Senegal), Sadio Mane (Senegal), Thomas Partey (Ghana) na Mohamed Salah (Egypt).

Shughuli za kupigia kura waliotajwa kupitia mitandao ya kijamii ilianza Jumamosi Novemba 17 na itafungwa rasmi Jumapili Disemba 2 kabla ya mshindi kutangazwa rasmi Ijumaa, Disemba 14.

Mshambulizi wa Liverpool raia wa Misri Mohamed Salah ndiye alishinda tuzo hiyo mwaka wa 2017, mwaka uliomshuhudia akihama Roma ya Italia hadi ligi ya EPL na baadaye  akaliongoza taifa lake kushiriki fainali ya kwanza la Kombe la Dunia tangu mwaka wa 1990.

Washindi wa awali wa tuzo hiyo inayohususdiwa mno ni Jay-Jay Okocha(Nigeria), Michael Essien(Ghana),  Didier Drogba(Ivory Coast), Yaya Toure(Ivory Coast) na Riyad Mahrez wa Morocco.

Mlinzi wa Atletico Madrid raia wa Ghana Thomas Partey ndiye mwaniaji ambaye hakushiriki fainali za kombe la Dunia mwaka huu huku wengine wote wakiwajibikia fainali hizo zilizoandaliwa nchini Urusi kati ya mwezi Juni na Julai mwaka 2018.