Michezo

Salah tayari kuongoza Liverpool kuzamisha chombo cha Atalanta kwenye UEFA baada ya kupona Covid-19

November 24th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

NYOTA Mohamed Salah amerejea mazoezini kwa minajili ya gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) litakalowakutanisha na Atalanta ya Italia uwanjani Anfield mnamo Novemba 25, 2020.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 alikosa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyoshuhudia Liverpool wakisajili ushindi wa 3-0 dhidi ya Leicester City uwanjani Anfield mnamo Novemba 22, 2020.

Kiini cha Salah kutokuwa sehemu ya gozi hilo ni ugonjwa wa Covid-19 alioupata wakati akiwa katika kambi ya timu ya taifa ya Misri iliyokuwa ikipepetana na Togo kwenye mechi mbili za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) mnamo 2022.

Hata hivyo, vipimo ambavyo fowadi huyo wa zamani wa Chelsea na AS Roma alifanyiwa vilibainisha kwamba amepona na akarejea mazoezini kujifua kwa gozi lijalo la UEFA.

Liverpool wanajivuia rekodi ya asilimia 100 kwenye kipute cha UEFA hadi kufikia sasa na watajikatia tiketi ya hatua ya 16-bora iwapo watawaangusha leo Atalanta inayoshiriki Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Miamba hao wa EPL wanajivunia kusajili ushindi katika mechi zao zote tatu katika michuano ya UEFA bila kufungwa bao lolote msimu huu, huku wakiendelea kufurahia uongozi katika Kundi D kwa tofauti ya pointi tano. Kundi hilo linajumuisha pia Midtjylland kutoka Denmark na Ajax ya Uholanzi.

Katika mechi iliyopita ya UEFA, Liverpool waliwapokeza Atalanta kichapo cha 5-0 jijini Bergamo, Italia na watajitosa ugani kwa minajili ya mchuano wa marudiano wakijivunia motisha ya kucharaza Leicester City 3-0 ligini.

Hata hivyo, huenda wakatolewa jasho na Atalanta hasa ikizingatiwa wingi wa visa vya majeraha kambini mwao. Kocha Jurgen Klopp atakosa huduma za wanasoka Trent Alexander-Arnold, Joe Gomez na Virgil van Dijk. Kadhalika, kuna uwezekano wa Jordan Henderson, Xherdan Shaqiri, Naby Keita, Thiago Alcantara na Alex Oxlade-Chamberlain kutocheza dhidi ya Atalanta.

Mbali na Salah, nyota wengine watakaotegemewa na Liverpool kwenye safu ya ushambuliaji ni Sadio Mane, Robert Firmino na Diogo Jota ambao waliridhisha sana dhidi ya Leicester City.

Licha ya kutokuwa maarufu, Jota ni miongoni mwa wafungaji mabao mengi katika michuano hii baada ya kufunga matatu katika mechi ya mkondo wa kwanza. Iwapo anafanikiwa kufunga dhidi ya Atalanta, atakuwa mchezaji wa kwanza wa Liverpool kuwahi kucheka na nyavu mara matatu katika michuano ya UEFA.

Kwingineko, Inter Milan wataialika Real Madrid ugani San Siro katika mechi ya Kundi B, huku Manchester City wakisafiri nchini Ugiriki kupambana na Olympiacos.

Borussia Monchengladbach wataalika Shakhtar Donetsk, FC Porto iwaendee Olympique Marseille nchini Ufaransa nao mabingwa watetezi Bayern Munich waikaribishe RB Salzburg ya Austria ugani Allianz Arena, Atletico Madrid na Lokomotiv Moscow watachuana uwanjani Wanda Metropolitano nao Ajax Amsterdam wawe wenyeji wa Midtjylland nchini Uholanzi.