Makala

Salasya alaumu shetani kwa ‘kumpotosha’

January 15th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

MBUNGE Peter Salasya wa Mumias Mshariki sasa amedai kwamba shetani ndiye amekuwa akimwingilia na kumfanya kujihusuisha na visa vya kushambulia watu wanaotofautiana naye.

Kwenye ujumbe alioandika katika ukurasa wake ‘X’ (awali Twitter), Jumapili, Januari 14, 2024, Bw Salasya alisema alikuwa akijutia vitendo vyake katika siku za hivi karibuni, kwani vimemharibia sifa na kutomfanya kuwa kielelezo chema kwa vjana.

Mbunge huyo pia alitangaza kuomba msamaha wakazi wa eneobunge lake na Wakenya kutokana na vitendo vyake.

“Mimi, Peter Salasya, ninaomba msamaha kwa watu wa Mumias Mashariki na Wakenya wote kwa jumla. Katika siku za hivi karibuni, vitendo vyangu havijakuwa vikinisawiri kama mfano bora kwa vijana. Kuanzia sasa, nitakuwa nikidhibiti hasira na vitendo vyangu. Ni shetani aki,” akasema.

Kauli yake, ‘ni shetani aki’ iliashiria ni shetani amekuwa akichangia kuwa na drama za vita kila wakati.

Katika siku za hivi karibuni, mbunge huyo amekuwa akijipata matatani, mara nyingi akibishana au kukabiliana na viongozi wenzake.

Mnamo Ijumaa, Januari 13, 2024 alikamatwa na polisi baada ya kumshambulia diwani (MCA) kwenye hafla moja ya mazishi katika Kaunti ya Kakamega.

Bw Salasya alikamatwa kwa dai la kumpiga kofi diwani Peter Walunya wa wadi ya Malaha/Isongo, na baadaye kuachiliwa kwa dhamana ya Sh50, 000.

Hapo kabla, mbunge huyo alikuwa amedai kwamba alikuwa “akimsalimia diwani huyo” wala si kumshambulia, kama ilivyodaiwa.

“Ningetaka kusisitiza kuwa yale mliyoyaona na kuyataja kama shambulio ni salamu katika lugha yetu. Ni desturi yetu ya kitamaduni,” akasema mbunge huyo.

Licha ya ombi hilo la msamaha, polisi walisema watamfikisha mahakamani Jumanne, wiki hii ili kujibu shtaka la kumshambulia mwenzake.

Mwaka uliopita, 2023 Bw Salasya alijipata kwenye visa kadha wa kadha akizozana na wakazi n ahata viongozi, akiwemo Gavana wa Kakamega Fernendes Barasa.