SALOME NJERI: Mtambue ‘Mama Chapo’ wa kipindi cha Maria

SALOME NJERI: Mtambue ‘Mama Chapo’ wa kipindi cha Maria

Na JOHN KIMWERE

INGAWA ndio ameanza kupata umaarufu katika sekta ya maigizo amepania kumiliki brandi yake ili kukuza talanta za waigizaji wanaokuja. Ni miongoni mwa wasanii wanaendelea kuvumisha kipindi pendwa cha Maria ambacho huzalishwa na kampuni ya Jiffy Pictures na kupeperushwa kupitia Citizen TV.

Salome Njeri Kiongo maarufu Mama Chapo anasema alianza kujituma katika masuala ya maigizo akiwa mtoto kipindi hicho akisoma darasa la tatu.

Kando na huigizaji dada huyu anamiliki kibanda katika kijiji cha Lindi Kibera ambapo hupika na kuuza miguu ya mbuzi maarufu ‘Futuku.’ ”Mamangu mzazi alinipiga sana kuwa kushiriki uigizaji ambapo nilikuwa nafanya kwa siri.

Hata hivyo nilipata nafasi kushiriki michezo ya uigizaji katika kanisa la St Michael Lang’ata,” anasema na kuongeza kuwa kwa sasa yupo tayari kushiriki filamu mbali mbali humu nchini huku akilenga kufikia upeo wa juu katika sekta ya maigizo.

Mwanzo wa ngoma anasema ili ajiunge na masuala ya uigizaji alivutiwa na filamu iliyoitwa ‘Tausi’ iliyokuwa ikipeperushwa kupitia runinga ya KBC. Pia anadokeza kuwa kunazo filamu zingine ikiwamo Moyo na Aziza zilizompangawisha zaidi.

Katika mpango mzima dada huyu amepata nafasi kushiriki kipindi cha Maria kilichoanzishwa mwaka 2019 pia kinachozidi kujizolea wafuasi kila kuchao.

Pia anajivunia kushiriki mara mbili katika kipindi cha ‘Varshita’ ambacho hupeperushwa kupitia Maisha Magic. Msanii huyu mama wa watoto wawili anasema angependa sana kutinga upeo wake msanii mzawa wa Marekani, Rachel Meghan Markle anaayejivunia kushiriki filamu nyingi tu kama ‘Suits.’

Kwa wanamaigizo wa kimataifa anasema angependa kujikuta jukwaa moja na wasanii mahiri katika filamu za Kinigeria (Nollywood) kama Mercy Johnson na Patience Ozokwor. Hapa nchini anasema angependa kufanya kazi na wasanii kama Naomi Ng’ang’a pia Catherine Kamau kati ya wengine.

Kando na changamoto za kawaida kwa wanamaigizo wengi ikiwamo kukosa ajira dada huyo anasema jamii inamchukulia tofauti hasa baada ya kuanza kushiriki kipindi cha maria.

”Dah!!!! Imekuwa vigumu sana kwangu kuabiri magari ya uchukuzi mitaani. Miongoni mwa wafuasi wangu katika kipindi cha Maria hudhania nina mkwaja mkubwa ambapo napaswa kuwa namiliki gari,” alisema na kuongeza kuwa hivi majuzi alipigwa na butwaa alipozuru katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta wafanyi kazi wengi hawakuamini kama anaweza kusaka matibabu katika hospitali ya kiwango hicho.

”Binafsi nashukuru mabosi wangu katika shirika la Royal Media kwa kunipa nafasi kuonesha kipaji changu katika uigizaji. Pia nashukuru Gazeti hili la Mwanaspoti kwa kuangazia wasanii wanaokuja ili kuwatia wengine moitisha,” akasema.

Dada huyu aliyezaliwa mwaka 1980 mtaani Kibera anasema tangia utotoni mwake alidhamiria kuhitimu kuwa mtangazaji kwenye redio ama runinga.

You can share this post!

RAEL ODIPO: Uigizaji si mzaha, lazima ujitume

CLARA VUGUTSA: Nalenga kuwapa mafunzo ya uigizaji wasanii...