Habari za Kitaifa

Samahani, nimefungwa mikono, Nakumicha aambia madaktari

Na LEON LIDIGU July 11th, 2024 1 min read

WAZIRI wa Afya, Susan Nakhumicha amesema hana uwezo wa kufanya maamuzi kuhusu ajira na malipo ya madaktari wanagenzi.

Alisema kwa sababu hiyo, serikali itaanza mara moja kuwatuma kazini madaktari wanagenzi 552 kwa kutumia kiwango cha malipo kilichopendekezwa na Tume ya Mishahara (SRC) cha Sh70,000 kwa mwezi, huku akisubiri uamuzi wa kesi iliyowasilishwa kortini Eldoret, kuhusu suala lilo hilo, ambao umeratibiwa kutolewa Septemba 26, 2024.

Akizungumza na Taifa Leo Jumanne jioni, Waziri aliwaomba radhi madaktari wote wanagenzi kwa uchungu, kusononeka, kuteseka kisaikolojia na mahangaiko ambayo wamestahimili kwa karibu miaka miwili.

“Wizara ya Afya (MoH) inafahamu athari hasi ambazo zimesababishwa na kuzidi kuchelewesha ajira ya madaktari wanagenzi,” alisema Waziri wa Afya.

“Tunasikitika kuhusu madaktari wetu wachanga ambao wamelazimika kustahimili mateso kisaikolojia na changamoto za kifedha huku tukijitahidi kutwa kucha kusaka suluhisho mwafaka kuhusu hali iliyopo,” alieleza kuwa, mgomo wa madaktari uliodumu kwa siku 56 ulishinikiza kubuniwa kwa mkataba wa kurejea kazini uliotiwa saini na serikali na muungano wa madaktari, Mei 8, 2024.

Waziri alifafanua kuwa, mkataba huo ulisheheni pendekezo kuhusu jinsi ya kutatua mgogoro unaohusu kuwatuma madaktari wanagenzi 1,210, suala tata likiwa kuhusu malipo ya wanagenzi.

“Japo KMPDU ilitaka wanagenzi waajiriwe kwa kutumia viwango vya mishahara vilivyowekwa katika Mkataba wa Malipo (CBA) 2017 vya Sh KES 206,400 kwa mwezi, uhalisia wa kifedha ikiwemo kufutiliwa mbali kwa Mswada wa Fedha 2024 hauwezi kuruhusu hili,” alisema Bi Nakhumicha.

Alisema pia kuna kesi kupinga agizo la SRC kuhusu malipo ya Sh70,000 na uamuzi utakaotolewa Septemba 26, 2024,.