Habari za Kaunti

Samaki Wakubwa: Mapapa wa unyakuzi wa ardhi Pokot Magharibi kukiona

May 3rd, 2024 2 min read

NA OSCAR KAKAI

WANYAKUZI wa mashamba katika Kaunti ya Pokot Magharibi wamemulikwa na serikali kuu pamoja na ile ya kaunti wakiambiwa chuma chao ki motoni.

Unyakuzi wa mashamba yanayorejelewa ulifanyika kinyume cha sheria miaka michache iliyopita kabla ya ugatuzi.

Watu mashuhuri, wenye ushawishi mkubwa na mabwanyenye kwenye kaunti hiyo wanasemekana kunyakua mashamba hayo makubwa ya umma kwenye miji mikubwa ya kaunti hiyo.

Hata hivyo, serikali kuu na ya kaunti zinawataka kuondoka mara moja kwenye mashamba hayo la sivyo wafurushwe kwa nguvu ili kuupa nafasi mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama ya chini.

Vilevile, serikali imetoa onyo kwa wale wanaokalia mashamba ya umma na mali nyingine za serikali katika kaunti ya Pokot Magharibi, ikisema kuwa inawakujia na itawang’oa bila notisi.

Kamishina wa Kaunti ndogo ya Pokot Magharibi Wycliffe Munanda alisema kuwa mpango wa nyumba za bei rahisi utaanza kwenye kaunti hiyo na serikali haitakawia kuwaondoa kwa nguvu wanaokalia vipande vya ardhi ya umma kinyume cha sheria.

“Historia ya mashamba inajulikana vyema. Yeyote anayeishi kwenye ardhi ya umma anafaa kuisalimisha. Mali ya umma ni mali ya raia,” akasema Bw Munanda.

Kulingana na Bw Munanda ambaye alizungumza wakati wa mkutano wa kushirikisha umma mjini Kapenguria kuhusu ujenzi wa nyumba za gharama ya chini, serikali inaangazia nyumba za bei nafuu ambapo Wakenya watapata fursa kuajiriwa kwenye kaunti na hata kunufaika kwa kupata nyumba hizo.

Waziri wa Ardhi katika Kaunti ya Pokot Magharibi Esther Chelimo ahutubia wanahabari mjini Kapenguria mnamo Mei 1, 2024. PICHA | OSCAR KAKAI

Waziri wa Ardhi wa Pokot Magharibi Esther Chelimo alithibitisha kuwa wametambua mashamba mjini Kapenguria ambayo yalinyakuliwa na ‘samaki wakubwa’ wanaoishi ndani wanafaa kuanza kufunga virago mara moja.

“Kuna wale ambao wako kwenye mashamba ya umma wakidai kuwa walipewa na baraza la kaunti. Tutafuatiliwa suala hilo,” alisema Bi Chelimo.

Naibu Mkurugenzi katika idara ya nyumba na ustawi wa miji nchini, Boniface Mule alisema kuwa serikali itaanza mpango wa nyumba za bei nafuu katika Kaunti ya Pokot Magharbi mara moja baada ya kukusanya maoni kutoka kwa wakazi akisema kuwa maoni hayo yatasaidia serikali kwenye mipango ya ujenzi.

Gavana wa Kaunti ya Pokot Magharibi Simon Kachapin aliwasuta mabwanyenye ambao wameiba mashamba ya umma katika eneo hilo hasa ardhi karibu na afisi za utawala na kwenye miji mikubwa.

“Tuko tayari kukabiliana nao na hawatahepa. Utajenga aje nyumba zao karibu na afisi za serikali?” aliuliza.

Aliongeza kusema kuwa serikali ya kaunti itawapokonya hatimiliki za mashamba ambayo ni ya umma na yalinyakuliwa kwenye kaunti hiyo.

“Mali nyingi ya umma imenyakuliwa na watu binafsi na wafanyabiashara. Majumba mengi ya kibinafsi yako kwenye mashamba ya umma ambayo yalinyakuliwa,” alisema Bw Kachapin.

Alisema kuwa baadhi ya watu walitumia ukora na kughushi stakabadhi kwa lengo la kuiba mashamba.

Bw Kachapin alitoa wito kwa taasisi za serikali kusaidia kurejesha mashamba ya umma ambayo yamenyakuliwa na watu binafsi ili eneo hilo liweze kunufaika na mpango wa nyumba za gharama ya chini.

“Suala la ardhi ni hatari na watu wengine wanaweza kutumia nafasi hiyo kujinufaisha kisiasa,” alisema.

Alisema kuwa ujenzi wa nyumba za gharama ya chini na mpango wa ujenzi wa soko katika kaunti hiyo utaimarisha ajenda ya maendeleo katika eneo hilo.

Maeneo ambayo yametambuliwa kujengwa nyumba hizo za gharama ya chini ni Bendera, Alale na katika ardhi ya gereza la Sigor.

Masoko yatajengwa kwenye miji ya Makutano, Alale, Ortum, na Sigor.

[email protected]