Habari Mseto

Samboja apokea mashine za kupambana na Covid-19

June 10th, 2020 1 min read

Na WINNIE ATIENO

HUDUMA za afya katika Kaunti ya Taita Taveta zimepigwa jeki baada ya kupokea mashine tano za kusaidia wagonjwa mahututi kupumua yaani ventilators.

Gavana wa Taita Taveta Granton Samboja amesema mashine hizo zitawasaidia katika juhudi za kupambana na ugonjwa wa Covid-19.

“Tumepokea mashine muhimu sana katika kupambana na virusi vya corona. Zililetwa na serikali kuu na zitatusaidia kutoa huduma kwa wagonjwa wa Covid-19 ambao wako mahututi. Zitaanza kutumika katika kipindi cha wiki moja baada ya kuwapa wahudumu wetu wa afya mafunzo,” akasema Bw Samboja.

Amesema serikali yake ya kaunti inafanya kazi kwa karibu na serikali kuu na mashirika mengine ili kupata maendeleo na kuimarisha sekta ya afya wakati huu ambapo ulimwengu unapambana na janga la corona.

Bw Samboja amesema vifaa hivyo vitapelekwa katika kituo malaum cha kutibu wagonjwa wa corona eneo la Mwatate.

“Vilevile kupitia mradi wa serikali kuu wa kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote maarufu Universal Health Coverage, tutapokea kliniki mbili tamba ambazo zitapelekwa eneo la Mililo huko Wundanyi na Njoro Masaini huko Taveta,” amesisitiza.

Gavana huyo amewasihi wakazi waendelee kufuata taratibu na maagizo ya Wizara ya Afya ili kuepuka virusi hivyo.?