Habari Mseto

Samboja: Mliopigia ‘ndio’ mswada tata naomba Mungu awasamehe, hamjui mlichotenda


ALIYEKUWA Gavana wa Taita Taveta Granton Samboja amewakemea wabunge wa kaunti hiyo waliounga mkono Mswada wa Fedha uliovukishwa bungeni Alhamisi. 

Akiongea mjini Mwatate, Bw Samboja alitaja wabunge hao kama wasiokuwa na huruma kwa wananchi wanaofinywa na gharama kubwa ya maisha inayosababishwa na ushuru wa bidhaa muhimu.

Katika kaunti hiyo, wabunge Lydia Haika (mwakilishi wa wanawake), John Bwire (Taveta) na Peter Shake (Mwatate) waliunga mkono mswada huo huku Danson Mwashako (Wundanyi) na Abdi Chome (Voi) wakiupinga.

“Bunge halina huruma na licha ya maandamano walipitisha huo mswada. Hayo ni makosa makubwa,” alisema.

Alisema mswada huo utaumiza wananchi wa chini ambao hawana uwezo wa kununua haswa chakula.

“Wameongeza ushuru kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ilihali vitu vingi vikiwemo mafuta tunaagiza nchi za nje. Tujitayarishe kwani hali ya maisha itakuwa ngumu huko mbeleni,” akasema.

“Mungu awasamehe wabunge waliounga mkono mswada huo. Hata mbunge wa hapa Mwatate alitushangaza alipounga mkono mswada huo lakini Mungu amsamehe na tuombee viongozi wetu,” akasema.

Wakati huohuo, mbunge wa Taveta Bw Bwire alitetea uamuzi wake na kusema kuwa aliunga mkono mswada huo kwa ajili ya maendeleo ya eneo lake.

Alisema licha ya kupigwa mawe kwa mkondo aliochukua, serikali ina lengo la kujenga barabara mbili kuu za eneo hilo na hivyo kumlazimisha kuunga mkono mswada huo.

Baadhi ya barabara zinazolegwa kujengwa ni ile ya Taveta-Eldoro-Mrabani na ya Cess-Jipe ambazo zitagharimu takriban Sh1.3 bilioni na Sh1.9 bilioni mtawalia.

Aidha alisema kuwa barabara ya Taveta-Illasit iko mpangoni kujengwa kwa Sh8.5 bilioni.

“Kipengele ambacho sikubaliani nacho ni ushuru wa barabara ambao uliongezwa kutoka Sh18 hadi Sh25. Hata hivyo, hizo pesa ndizo zitajenga hizi barabara kwa hivyo nitapingaje?” akasema.

Akiongea katika eneo la Rekeke mjiji Taveta, alisema kuwa wengi wanaopinga mswada huo hawajausoma.

“Nilisoma mswada huo na ile ripoti ya Kamati ya Bunge ya Fedha ndipo nikatoa uamuzi wangu. Yule aliyesoma ripoti hiyo hapa anyoshe mkono juu. Nasikia mnasema kuwa mlinituma nikapinge mswada huo lakini yule ana sababu yake aniambie,” akawaambia wenyeji.

Aidha alisema ushuru huo wa barabara hautaathiri wananchi ambao hawana magari.

“Acheni matajiri kama mimi Bwire tulipe hiyo kodi. Hata hivyo mkisema hamtaki niunge mkono mswada huo Jumanne nitapiga la,” akasema.