Samia Suluhu Hassan aapishwa kuwa Rais wa sita wa Tanzania

Samia Suluhu Hassan aapishwa kuwa Rais wa sita wa Tanzania

Na SAMMY WAWERU

BI Samia Suluhu Hassan ameapishwa rasmi Ijumaa kumrithi Rais Dkt John Pombe Magufuli aliyefariki Jumatano.

Bi Samia amekula kiapo katika Ikulu ya Rais jijini Dar es Salaam, iliyoongozwa na Spika wa Bunge la Tanzania, Bw Job Ndugai.

“Nitakuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…Nitazingatia Sheria za Katiba…Nitawatendea haki Watanzania wote bila mapendeleo,” akasema Bi Samia, akiahidi kuiongoza Tanzania kwa hali na mali katika kipindi cha muda uliosalia Dkt Magufuli akamilishe awamu ya uongozi.

Hadi kufikia kifo cha Rais Magufuli, Bi Samia amekuwa Makamu wake. Aidha, Bi Samia atakuwa Rais wa sita wa Tanzania na Rais wa kwanza mwanamke kutawala nchi hiyo.

Vilebile, atakuwa Rais wa kwanza mwanamke kuwa madarakani katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki.

Kinyume na sherehe za Rais kuapishwa nchini Tanzania, hafla ya Bi Samia kula kiapo imeendeshwa chini ya muda mfupi ambapo haikuwa na mbwembwe nyingi kwa mujibu wa taratibu, mila na itikadi za taifa hilo.

Baada ya kuapishwa, kikosi cha kijeshi Tanzania kimefyatua mizinga kama heshima kumlaki kuingia Ikulu.

Bi Samia pia amekagua gwaride la wanajeshi. Marais wastaafu, Mabw Hussein Ali Mwinyi na Jakaya Mrisho Kikwete wamehudhuria hafla hiyo.

Tawasifu

Samia alizaliwa Januari 27 mwaka 1960 visiwani Zanzibar, anakuwa Rais wa kwanza Tanzania kuongoza Serikali baada ya mtangulizi wake kufariki akiwa madarakani.

Samia alisoma shule kadhaa za msingi kabla hajahitimu Mahonda iliyopo Unguja mwaka 1972 kisha akajiunga na Sekondari Ngambo na Lumumba hadi mwaka 1975. Mwaka 1977 Samia alijiunga na Taasisi ya Fedha na Utawala Zanzibar (ZIFA) alikotunukiwa cheti cha takwimu na kuajiriwa na Wizara ya Mipango na Maendeleo.

Baadaye alijiendeleza katika Taasisi ya Maendeleo na Utawala Mzumbe (IDM) ambayo sasa ni chuo kikuu kwa stashahada ya utawala.

Mwaka 1978 Samia aliolewa na Hafidh Ameir ambaye wakati huo alikuwa ofisa kilimo na mwaka 1989 alijiunga na Chuo cha Taifa cha Usimamizi na Utawala wa Umma cha nchini Pakstan kwa masomo ya utawala na mwaka 1991, alienda kusomea utawala kwa viongozi katika Chuo cha Hyaerabad nchini India.

Mwaka 1992, Samia aliajiriwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kisha akaenda Chuo Kikuu Manchester, Uingereza kwa masomo ya stashahada ya juu ya uchumi.

Samia pia ana shahada ya umahiri katika maendeleo ya uchumi aliyoisoma Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na Chuo Kikuu cha Southern New Hampshire cha Marekani.

Mwaka 2000 Chama cha Mapinduzi (CCM) kilimteua kuwa mwakilishi kupitia Viti Maalumu na akiwa kwenye Baraza la Wawakilishi aliteuliwa na Rais Amani Karume kuwa waziri.

Mwaka 2005 aliteuliwa tena hadi mwaka 2010 alipogombea ubunge katika Jimbo la Makunduchi alikoshinda kwa asilimia 80. Baada ya uchaguzi huo aliteuliwa kuwa Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais kushughulikia Muungano.

Mwaka 2014, Samia alichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba lililoandaa Rasimu ya Katiba Mpya.

Jumapili ya Julai 12 mwaka 2015, Dk John Magufuli alipopitishwa kuwa mgombea wa urais wa CCM, Samia alikuwa mgombea mwenza.

Katika kinyang’anyiro cha ndani ya chama kilichoongozwa na Rais Jakaya Kikwete aliyekuwa mwenyekiti aliyemuelezea Dk Magufuli kama kiongozi mchapakazi, makini na asiyependa uvivu, kilimaliza makundi yaliyokuwapo kabla.

Kwenye kinyang’anyiro hicho, Dk Magufuli alipata kura 2,104 sawa na asilimia 87.08 hivyo kukabidhiwa bendera ya njano na kijani kukiwakilisha chama hicho na baada ya kunadi sera vilivyo, CCM ilishinda, Samia akaapishwa kuwa Makamu wa Rais.

You can share this post!

Utawala wa Magufuli ulikandamiza haki za kibinadamu

Rais Suluhu awahimiza Watanzania kuungana