Bambika

Samidoh: Hizi drama zangu nazipenda sana, zinanipa hamu ya kuishi

April 7th, 2024 2 min read

Na SINDA MATIKO

STAA wa mugithi, Samuel Muchoki, almaarufu Samidoh anasema anayahusudu maisha anayoishi pamoja na drama zote za wanawake anaohusishwa nao.

Samidoh ana watoto na mke wake wa zamani Edday Nderitu pamoja na Seneta Karen Nyamu. Wanawake hao mara si moja wamekuwa wakizua drama wakiligombania penzi la Samidoh.

Mwisho wake staa huyo huishia kutrendi kwa visanga vyake hivyo na ndio yamekuwa maisha yake.

“Kama singelikuwa nayapenda maisha ninayoyaishi mimi, ningelikuwa nimeshajitia kitanzi zamani sana. Nimejifunza maisha yana changamoto zake ila la msingi ni kusalia kwenye mstari na kusonga nayo,” Samidoh kafunguka.

Ni mtazamo huu wa kimaisha ambao sasa umemfanya Samidoh kupenda kutrendi.

“Sidhani kutrendi ni vibaya. Mwenyewe huwa najikuta tu nimetrendi pasi na kujua chanzo. Hata mabosi wangu kufikia sasa wameshaelewa haya ndio maisha ninayoishi hivyo huwa sina kesi nao,” ameongeza.

Samidoh ambaye ni afisa wa polisi, aidha anasisitiza kuwa ameshakubali kuwa ustaa una gharama yake.

“Kuna gharama ya kulipiwa kwa kila kitu. Kipindi nilikuwa nachunga ng’ombe kule Ol Jorook singewahi kutrendi maana nilikuwa mtu wa kawaida sana. Lakini sasa mimi ni maarufu hivyo lazima wakati mwingine patazuka taarifa hasi ila la muhimu ni kujua namna ya kubalansi. Drama zitakuwepo na pia kutakuwepo na matukio mazuri na kikubwa cha kufanya ni kutojali unavyopondwa kwa matukio ya drama.”

Aidha, Samidoh kafunguka kuhusu utendaji wake kazi jambo ambalo limekuwa likiwakanganya wengi kutaka kufahamu ni wakati gani anafanya ajira maana muda mwingi anaonekana akiwa kwenye matamasha na hafla za burudani.

“Huwa nafanya kazi kutoka Jumatatu hadi Alhamisi halafu sasa nakutana na mashabiki kutoka Ijumaa mpaka Jumapili. Nina bosi mzuri ambaye anaamini sana katika kipaji changu na ndio maana huwa napewa nafasi ya kwenda kukionyesha. Hata ninapokuwa nimepata shoo nje ya nchi mabosi wangu huridhia kabisa kwa hiyo kikazi niko sawa. Sijawahi kuihatarisha,” ameongeza.

Kuhusu matunzo ya wanawe ishu nyingine ambayo amekuwa akipondwa sana na wanawake wake kwamba katelekeza baadhi ya wanawe, Samidoh anapinga.

“Inawezekana mimi sio vitu vingi ila kimoja ninachoweza kukuhakishia ni kuwa mimi ni baba mzuri. Nipo kwenye maisha ya watoto wangu wote iwe kifedha, kisaikolojia nipo.”