Makala

SANAA: Mwanamuziki wa Injili anayetangaza huduma maarufu ya uchukuzi wa teksi

May 19th, 2020 3 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

MAMAKE alimzaa akiwa angali katika shule ya upili. Akiwa ndiye mtoto wa pekee anayelelewa na mzazi mmoja – mama – Amos Njoroge maarufu MC Emos amepata ushabiki na uungwaji mkono katika tasnia ya burudani.

Kwa sasa ni kijana mwenye umri wa miaka ambayo ndiyo inagonga 30 tu, lakini ana sifa aina na ainati; ni mwanamuziki wa Injili; anajivunia ufuasi mkubwa wa wafuasi katika mitandao ya kijamii; ni mpanga tafrija, mpigapicha, mtangaza huduma maarufu ya uchukuzi wa teksi kimtandao ifahamikayo kama ‘Wasili’ ambayo shughuli zake zinaenda kufanana na zile za Uber na Taxify.

Kwa sasa teksi za ‘Wasili’ zinahudumu mjini Nakuru.

Kijana huyu pia hakosi kujiita balozi wa parachichi – nafasi iliyochangia aanze kutengeneza nguo nzito zenye kofia maarufu ‘Hoodies’ na T-shirts anazochapisha nembo au lebo safi aliyoipa jina #AvocadoRepublik kukiwa na picha maridadi ya parachichi.

Emos ni mzawa wa Nakuru ambaye pia amekulia kuko huko.

Mara baada ya kukamilisha elimu yake ya sekondari, msanii huyu alijiunga na taasisi ya masomo ya Uanahabari ya Afrika Mashariki, East Africa Media Institute. Ni akiwa katika taasisi hii ambapo alijihami barabara na ujuzi wa kurekodi na kuhakiki picha za video.

Kazi hii imemwezesha kukidhi mahitaji yake muhimu ikiwa pamoja na kumwezesha kula kwa kijiko ikizingatiwa kwamba ni ujuzi ambao umemkutanisha na nguli wa burudani kama Avril, King Kaka, na Groove Networks.

Mwaka 2011, Emos alipata wazo la kuwainua vijana nyumbani Nakuru kwani limbukeni walioonyesha kujituma walikuwa ni wengi kibao.

Basi aliona ingekuwa bora paundwe vuguvugu la kuwaleta vijana pamoja na kujikubali kama wenyeji na wakazi wa Nakuru. Kwa hili, aliamua kuanzisha kauli kama ‘Nakuru Stand Up (NSU)’ kumaanisha Nakuru Simama ambapo uungwaji mkono ulikuwa mkubwa mno.

Amos Njoroge maarufu MC Emos. Picha/ Margaret Maina

.“Wasanii wengi Nakuru wanatambua na kujihusisha na Nakuru Stand Up,” asema MC Emos .

NSU imetoa mchango mkubwa wa kuboresha maisha ya wakazi hasa kupitia miradi inayolenga kuirudishia jamii shukrani.

Mradi mmojawapo ni ule wa ‘Lishana Vishana’ unaolenga wasiobahatika katika jamii ambapo chakula na mavazi yanatolewa kwa ajili ya kunufaisha wasiojiweza. Vilevile kuna hotuba zinazotolewa mahusi kwa makundi kama haya kwa ajili ya kuwapa watu motisha na kujirudishia imani ya kwamba “bado tunaweza kujinyanyua kuboresha hali zetu.”

Mradi mwingine wa vuguvugu hili ni ule wa ‘Pink City Reaction’, ambao una ufuasi mkubwa kutoka kwa vijana wanaopenda kujaribu vitu vipya. Dhamira ya Pink City Reaction ni kuimarisha sekta ya utalii hasa wa nyumbani ambapo vijana wanajihusisha na usafiri na ziara za kujionea hiki na kile kufurahisha macho na kujipa msisimko kwa kufurahia kazi ya Mungu pamoja na kutambua shughuli za binadamu katika Sayari hii ya Dunia.

‘Pink City’ ni jina lililoundwa ikiwa ni kutambua uwepo wa ndege aina ya flamingo ambao ni kivutio kikubwa cha utalii katika Ziwa Nakuru.

Emos anasema haiwi tatizo kwake kushirikisha shughuli na program zote.

“Naipenda sanaa hivyo inakuwa rahisi kwangu kufanya kulihali kuimarisha vipaji Kaunti ya Nakuru,” asema.

Emos aliwahi kufanya kazi ya kuwasilisha vipindi kwa muda wa miaka mitatu katika redio ya hapo Nakuru iitwayo Hero Radio. Akiwa hapo sauti yake ilimpa umaarufu miongoni mwa mashabiki na ikawa ni lulu ya kufanikisha yeye kuwaleta studioni na kutangamana na majina kubwa katika tasnia ya burudani kama Rayvanny, Harmonize, Rich Mavoko, Alaine and Sauti Sol.

Mwaka 2015 Emos alishinda tuzo ya Flamingo Award—tuzo ya kila mwaka inayotambua juhudi za wasanii mjini Nakuru—kategoria ya Mwasilishaji Bora wa Kiume wa Redio.

Mwaka mmoja baadaye aliacha kazi katika kituo cha redio akilenga kujiimarisha zaidi na kuinua brandi yake.

“Nililenga kukua na kuitambulisha brandi yangu,” anaelezea.

Mara baada ya kujiuzulu, alianzisha shoo ya mtandaoni ya Mc Emos O’clock, ambapo kila Alhamisi anapeperusha mubashara katika ukurasa wake wa Facebook mahojiano kati yake na wasanii mbalimbali hasa wale ambao ndiyo mwanzo wanainukia.

Akiwa ni mpenda bidhaa na huduma za nyumbani, Emos aliamua kurekodi na kupeperusha tangazo la huduma ya teksi kwa njia ya kubonyeza simu iitwayo Wasili, hata bila ya kulipisha watoa huduma yenyewe na kisha kuichapisha katika mitandao ya kijamii.

Ni hatua iliyofanya waasisi kumpa kazi ya kuwa balozi wa kuitangaza Wasili.

“Wasili imeleta sura mpya ya usafiri katika eneo la Rift Valley ambapo kwa kubofya tu simu, abiria anapata chombo cha usafiri,” asema.

Kwa sasa kazi yake ya MC na utumbuizaji ndiyo chanzo kikubwa cha kipato chake. Anajipa kiasi cha kati ya Sh80, 000 na Sh120, 000 kutegemea ni msimu gani.

Ingawa ameshirikiana na wasanii wa nyimbo za kiulimwengu zaidi, azma yake ni kuitangaza Injili kupitia muziki.

Aidha, Emos ni shabiki sugu wa mavazi ya Kiafrika na tayari ni mmoja wa watangaza lebo ya CalvoCarlWear wanaotengeneza mavazi ya Kiafrika.

“Nguo anazovaa msanii ni njia moja ya kutangaza bidhaa za nyumbani,” asema.

Kwa sasa azma yake msanii huyu ni kuhakikisha ‘MC Emos O’clock ni inakuwa ni huduma ya utangazaji inayojikita zaidi kwa mtandao wa Facebook pamoja na kuwa na chaneli yake katika mtandao wa video na sauti wa YouTube.

Emos ananuia kutunga na kuimba pamoja na kuzalisha nyimbo nyingi akitafakari pia kuunda kampuni ya kutangaza na kuinua upeo wa bidhaa na huduma za wateja wake.

Msukumo uliomfikisha alipo ni: “Si kile unachokifanya, ni jinsi ambavyo unakifanya.”