Makala

SANAA: Shamir afurahisha mashabiki kwa muziki wake wa mapigo ya reggae

January 6th, 2020 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

MSANII Abdallah Mohamed ‘Shamir’ ametambulika kwa wimbo wake wa hivi punde ujulikanao kama ‘Me too’ ambao una mapigo ya mtindo wa reggae.

Wimbo huu ambao aliutambulisha sokoni mwaka 2019 na umekuwa ukichezwa kwenye vyombo vya habari mbalimbali nchini na mitandaoni.

Mbali na kibao hicho, Shamir amekuwa akitunga nyimbo zingine katika mtindo huo ambazo zimewavutia wapenzi wa aina hiyo ya muziki.

Shamir anasimulia safu hii kuwa aliamua kufanya muziki ili kujiepusha na mazingira hasi ambapo kulikuwa na utumizi wa dawa za kulevya ambazo zilichangia katika kuharibu maisha ya vijana eneo lake la kuzaliwa na kulelewa.

“Haikuwa rahisi kuamua kufanya vitu tofauti hasa katika mazinbgira yaliyokuwa na ushawishi mkubwa wa matumizi ya mihadarati,” anasema Shamir.

Ingawa hivyo, alipokuwa akisoma, Shamir alitamani sana aje awe afisa wa polisi.

“Nilibadilisha ndoto yangu baada ya kutunga wimbo ‘On Fire’ ambao ulivuma nikiwa katika shule ya upili. Ni hapo ndipo niliamua niwe mwanamuziki, akasema Shamir wakati wa mahojiano.

Alipokamilisha elimu yake ya shule ya upili, alijiunga na chuo cha Homeboiz Music Technology Academy ambapo alisomea taaluma ya uzalishaji muziki na utambuzi wa sauti yaani ‘Music production and sound engineering’.

Baada ya kupokea mafunzo hayo, alijunga na wanamuziki mbalimbali nchini ambao walikuwa tayari wanafanya muziki amabao walimsaidia katika kuikuza talanta yake.

Kufikia sasa, Shamir amefanya kazi na wasanii mbali mbali nchini haswa kama produza.

“Ninapenda sana mtindo wa reggae kwani hizi ni nyimbo ambazo hazipitwi na wakati na zinavutia watu wa aina mbalimbali kote ulimwenguni,” akasema Shamir.

Anawahimiza wasanii wenzake kufuatilia vipaji vyao na kuwa na msimamo ili kuhakikisha mashabiki wanaunga mkono kazi zao.

“Ni vizuri kuwa na mtindo ambao unatambulika nao, mashabiki pia wataweza kushabikia kazi yako bila ugumu wowote,” anaongeza Shamir.