Habari MsetoSiasa

Sanamu za Sonko zaharibiwa jijini

February 26th, 2020 1 min read

Na MARY WANGARI

WAKAZI wa kaunti ya Nairobi jana walishangaa kupata sanamu za simba zilizowekwa na Gavana Mike Sonko katika kiingilio cha wageni mashuhuri katika Baraza la Jiji, zikiwa zimeharibiwa na watu wasiojulikana.

Picha za sanamu hizo zilizosambazwa mno mitandaoni jana zilionyesha sanamu moja ya simba ikiwa imejaa masizi meusi ya moshi huku mchongo mwingine ukiwa na maandishi na kupakwa rangi tofauti.

Wakazi na wapita njia walisalia na maswali tele bila majibu huku baadhi ya maafisa wa kaunti wakionekana wakipakia michongo hiyo iliyoharibiwa kwenye lori la kaunti.

Taifa Leo ilipowasiliana na afisa wa mawasiliano katika Kaunti ya Nairobi, Bw Jacob Elkana, alithibitisha kisa hicho huku akisema maafisa wa upelelezi walikuwa wamearifiwa.

Kulingana na afisa huyo, sanamu hizo ziliharibiwa mnamo Jumanne jioni na watu wasiojulikana.

“Tuna wasiwasi. Hata sisi hatujui walioharibu michongo hiyo. Lakini tumeripoti kwa maafisa wa upelelezi,” alisema Bw Elkana.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo jana ulibainisha kwamba ni michongo iliyo nje ya Baraza la Jiji pekee iliyoharibiwa na kuondolewa.

Hali ilikuwa shwari kwa michongo ya simba mingineyo iliyowekwa katika maeneo mengine jijini humo.

Tukio hilo lilijiri saa chache tu baada ya gavana huyo wa kaunti ya Nairobi anayekabiliwa na wakati mgumu, kutia sahihi mkataba wa kuhamisha baadhi ya majukumu muhimu ya kaunti kwa Serikali ya Kitaifa.

Hatua hiyo iliyofanyika Ikulu Jumanne, iliashiria mkondo mpya kuhusu usimamizi wa jiji kuu nchini.