Habari

Sanitaiza ya BBI yang'arisha Waiguru

June 27th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

MSIMAMO wa Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru kuhusu handisheki na Mpango wa Maridhiano (BBI), umetajwa kama uliomwokoa na hivyo kumwepusha kwenda nyumbani.

“Sio kwamba madiwani wa Kirinyaga hawakuwa na ushahidi wa kumtimua Waiguru. Aliponyoka kwa sababu anaunga mkono ajenda ya walio na mamlaka ambao waliamrisha washirika wao katika Seneti kumtakasa,” asema mchanganuzi wa siasa, Wakili Peter Oluoch.

Anaongeza: “Thibitisho ni madai ya Kiongozi wa Wachache katika Seneti, James Orengo ambaye ni mwandani wa Bw Odinga, aliyedai Waiguru anaandamwa na watu walio nje ya bunge la Kaunti ya Kirinyaga.”

Kulingana na Kiongozi wa Narc-Kenya Martha Karua, viongozi wanaounga mkono handisheki na BBI wanakuwa na uhakika wa kuondolewa madai ya uvunjaji sheria kinyume na inavyowatokea wanaopinga.

“Tangu mwanzo, ilikuwa wazi Seneti ingemtakasa Waiguru kwa kuhusisha masaibu yake na maadui wa handisheki na BBI. Baada ya kutimuliwa na madiwani wa Kirinyaga, ilidaiwa alikutana na kiongozi wa ODM Raila Odinga. Kilichofuata ni washirika wa Odinga kuahidi kumuunga mkono,” akaeleza Bi Karua.

Aliongeza: “Odinga ni kinara wa handisheki akiwa na Rais Uhuru Kenyatta na BBI ni mtoto wao. Sio siri wamekuwa wakiwatetea wanaoiunga mkono.”

Mara baada ya MCAs wa Kirinyaga kupiga kura kwa wingi kumtimua gavana wao, Mbunge wa Suna Mashariki ambaye mwandani wa karibu wa Bw Odinga, Junet Mohamed alitangaza kuwa watasimama na Bi Waiguru kwa hali na mali, kauli iliyoonyesha ODM ilifikia uamuzi hata kabla ya kusikiza hoja za watu wa Kirinyaga.

Kutimuliwa kwa Bi Waiguru kulifika Seneti siku chache baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuwatema maseneta wanaopinga BBI kutoka nyadhifa za uongozi.

Hii ilisaidia UhuRaila kuhakikisha kuwa kamati ya kuchunguza madai dhidi yake ilijumuisha wanachama wenye msimamo wa kirafiki kwa gavana huyo.

Viongozi wa wengi na wachache pamoja na viranja wa pande zote mbili ndio wanaoteua wanachama wa kamati ya kusikiliza madai ya madiwani dhidi ya gavana, hali iliyomfaa Bi Waiguru.

“Uamuzi kuhusu Waiguru uliafikiwa kamati ilipoundwa. Kwa hivyo, kutakaswa kwake sio habari mpya,” alisema Seneta Kipchumba Murkomen wa Elgeyo Marakwet.

Muungano wa kutakasa wasakataji ngoma ya handisheki na BBI pia ulipata nguvu baada ya Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka kuuza imani yake kisiasa kwa Jubilee wiki chache zilizopita.

Ishara nyingine kuwa handisheki na BBI zilikuwa nyuma ya gavana huyo pia ilitoka kwa Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu) Francis Atwoli, ambaye aliwahimiza vinara wa mchakato huo kumuokoa Bi Waiguru.

Ishara kuwa mchakato wa kuchunguza madai dhidi ya Bi Waiguru ilikuwa shughuli ya kuonyesha wananchi kuwa sheria imefuatwa, ilijitokeza tangu hoja ilipowasilishwa, na maseneta wakaamua kutumia mtindo kinyume na uliomng’oa madarakani aliyekuwa gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu.

Bw Waititu kisiasa aliegemea mrengo wa Naibu Rais William Ruto, na wakati huo ushirika wa handisheki na BBI uliungana kumfukuza madarakani.

Kwa kuweka siasa za handisheki na BBI mbele ya matakwa ya wakazi wa Kirinyaga, kamati hiyo iliyoongozwa na Seneta Cleophas Malala wa Kakamega, ilifumbia macho madai ya ufisadi na kusema kwamba tofauti kati ya Bi Waiguru na madiwani ni za kiusimamizi.

Hata hivyo, kamati hiyo ilialika Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) kufuatilia madai ya madiwani hao dhidi ya Bi Waiguru.

Kulingana na wadadisi, hii inaonyesha kwamba uamuzi wa kamati ya Bw Malala ulikuwa wa kisiasa.

Kwenye taarifa yake ya mwisho kwa kamati hiyo, Bi Waiguru alisema masaibu yake yamechochewa na viongozi kutoka nje ya Kirinyaga wasiofurahishwa na hatua yake ya kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta kufanikisha BBI na handisheki yake na Bw Odinga.