Habari Mseto

Sankok na mapenzi kwa mkewe

September 28th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

MBUNGE maalum wa Jubilee David Ole Sankok, pengine ndiye mwanamume stadi zaidi wa mapenzi jijini baada ya kumtuza mkewe Hellen Seyianoi Sankok gari huku akimmiminia sifa tele kwa kusimama naye hata alipokuwa hana hanani.

Sankok alijitosa katika mtandao wa kijamii wa Facebook mnamo Ijumaa ambapo kupitia shairi la kutekenya hisia, alielezea mapenzi yake ya dhati kwa barafu ya moyo wake huku akimshukuru kwa kumchagua alipokuwa bila chochote cha kumpa ila Sh5 na ucheshi.

“Ninapokukabidhi zawadi hii spesheli ya gari, nakumbuka siku tulipojivinjari Uhuru Park. Sikuwa na pesa ila Sh5 mfukoni mwangu ambazo zilitosha tu kununua ice cream mbili,”

Akaongeza: “Nakumbuka hatukuwa tumekula chamcha. Si kwamba hatukua na njaa bali kwa sababu mifuko yangu ilikuwa mitupu, Sikuwa na hela ila ndoto nyingi na zawadi maalum; ucheshi.”

Baba huyo wa watoto saba alimpongeza mkewe kwa kuacha mali ya babake na kumfuata licha ya kuwa kilema na wanaume wengi waliokuwa wakimmezea mate.

“Uliacha nyumba ya babako ya mawe, magari mawili ya Datsun na Chevrolet, lori la Toyota, na trekta tatu katika boma la babako. Wewe huyooo ukamfuata kijana mlemavu kwangu nikiwa na shoka na upanga kama mashine zangu kubwa zaidi. Kumbuka enzi hizo msichana mrembo katika jamii ya Wamaasai alikuwa dhahabu, wanaume wote, wazee kwa vijana walijitahidi,” akasema.

Kukosa muda

Aidha, alimwomba radhi mkewe kwa nyakati alizojishughulisha zaidi na siasa na kukosa kuwa na muda naye.

“Huenda katika shughuli zangu nyingi kama mwanasiasa nilisahau kuimba nyimbo tamu na kukariri maneno matamu. Nyakati nyingine najishughulisha zaidi na biashara zetu badala ya kukupa muda unaostahili. Wakati mwingine nafikiri siimbi vya kutosha jinsi nilivyofanya miaka iliyopita, nyakati nyingine nafikiri sikariri maneno ya mapenzi kila mara vya kutosha,” akasikitika.

Mbunge huyo majuzi alieleza majuto yake kwa kujiunga na siasa akitangaza mipango ya kustaafu mapema kutoka ulingo wa siasa aliofichua umemwathiri kifedha.

Aidha, alifichua kuwa hatua hiyo itampa muda wa kutosha kukaa na familia yake na kushughulikia biashara zake huku akiangazia wadhifa muhimu katika Umoja wa Mataifa.