Bambika

‘Sapraizi’ ya Terence kwa mkewe Milly Chebby

February 8th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

MCHESHI Lawrence Macharia almaarufu Terence Creative amempa mkewe Milly Chebby zawadi ya Sh300,000 kuonyesha walivyotoka mbali tangu ampe pete ya Sh3,000 miaka kadhaa iliyopita.

Kwenye ukurasa wa Facebook, baba huyo wa watoto watatu alipakia ujumbe wa kumshukuru Mungu kwa kumwezesha kununua zawadi za kumpa mkewe aliyekuwa akisherekea miaka 37 ya kuzaliwa.

Pia, alichukua fursa ya kujikumbusha kuwa na matamanio ya maisha ya raha yenye kazi nzuri yenye mapato ambayo yangemwezesha kutimiza ndoto hizo kwa mkewe.

 “Miaka kadhaa iliyopita, nilikuwa na uwezo wa kununua pete ya Sh3,000 pekee kukuposa. Nashukuru Mungu nina uwezo wa kukupa zawadi ya Sh300,000,” alipakia Terence Creative.

 “Babe furahia hii zawadi ya simu aina ya iPhone 15 pro max 1tb… Kwa mpango mzuri nitalipa polepole mpaka tumalizane,” alisema kwa kucheshi.

Kando na zawadi hiyo, ndoto ya Milly Chebby kusherekea siku yake ya kuzaliwa Afrika Kusini iliweza kutimia mwaka huu.

Hii ni baada ya mcheshi hiyo kupakia video ya dakika 12 wakiwa kwenye ziara kwa kutumia ndege aina ya helikopta na gari aina ya cruise.

“Hii ilikuwa mojawapo ya orodha yangu mwaka huu. Kwanza tuliona Mlima Jedwali, kisha Kichwa cha Simba na kilele cha Chapman. Pia tuliona Cape Point, ambayo tulitembelea hapo awali na Robben Island,” alichangia Milly Chebby kwenye chapisho la mumewe.

“Pia tuliona Uwanja wa Cape Town, ambao uliandaa Kombe la Dunia mwaka wa 2010, na nilifurahi sana. Niliweza kuutazama kutoka juu,” alishiriki Milly Chebby.

Milly Chebby ni miongoni mwa watu maarufu waliotunukiwa zawadi ya simu ya aina hiyo baada ya Diana Marua kutunukiwa na mumewe mbele ya umma Desemba 2023 kwa kusherekea miaka saba kwenye ndoa.