Bambika

Sarah afichua sababu ya kukatalia mbali penzi la Diamond Platnumz

May 1st, 2024 2 min read

NA SINDA MATIKO

BAADA ya Diamond Platnumz kumtambulisha rasmi ex-wake Sarah aliyemfanya kuitunga hiti yake ya kwanza ‘Kamwambie’ iliyoishia kumtoa na kumfanya awe staa aliye kwa sasa, mrembo huyo ametia neno kuhusu yalivyokuwa mahusiano yao.

‘Kwamwambie’ iliyotoka 2009, ni simulizi ya kweli ya mateso ya kimapenzi aliyopitia Diamond baada ya kukataliwa na Sarah.

Juzi akitumbuiza kwenye shoo ya Serengeti Fiesta, Diamond alimpandisha stejini na kurudi miaka 15 nyuma kipindi alipokuwa akimtaka kimapenzi kabla hajatoka.

Mbele ya hadhira iliyokuwepo kwenye shoo, staa huyo alisimulia jinsi alivyokuwa akimpenda sana Sarah na ndio maana aliumizwa sana mrembo huyo alipomkataa kiasi cha kumpelekea kuingia studio na kutoa ‘Kamwambie’ iliyogeuka kuwa hiti na  utambulisho wake kwenye gemu la muziki.

Kwenye ‘Kamwambie’ Diamond analilia penzi la Sarah huku akimtahadharisha kuwa ajihadhari na watu wenye pesa wanaomfuatilia, anachodai kuwa ndio chanzo cha mrembo huyo kumkataa kwa kuwa yeye hana uwezo huo kama ilivyokuwa kwa wakati huo.

Diamond alidai kuwa Sarah alimchapa ‘matukio’ ya kutosha yaliyomuumiza sana moyo kuelekea yeye kumkataa kabisa.

Lakini Sarah akinyoosha mambo, alikiri kuwa Diamond anajua kupenda na kwamba akimpenda mwanamke, anampenda kwelikweli.

“Nasib hana maudhi, muulize mwanamke yeyote wa Nasib hana maudhi, ni mjinga kwanza kwenye mapenzi, huwa anapenda sana, akimpenda mwanamke  anamfanyia kila kitu, yani kila kitu mwanamume anapaswa kumfanyia mwanamke wake kumdekeza na nini, hana maudhi kabisa (navyo),” Sarah alimpa Diamond maua yake.

Hata hivyo Sarah alikuwa mwepesi wa kukana kuwa alifanya maksudi  kumchapa Diamond matukio akisisitiza kuwa tabia za michepuko za Diamond ndizo zilizomfanya amkatae.

“Hana maudhi akimpenda mwanamke, labda uongo uongo tu ingawa yeye anasema nimemfanyia vitu vingi (kumpiga matukio) ila hata yeye kuna vitu alikuwa anafanya ambavyo sijawahi kusema. Nasibu ana uongo uongo wa mapenzi… anakudanganya kitu halafu unakuja kujua. Nasibu ku-cheat ni toka zamani. Wewe si Nasib unamjua ku-cheat kwake ni lazima… Ila alikuwa ananipa kipaumbele… alikuwa anawaambia wanawake wake hao (michepuko) kunihusu mimi ila Nasib hana maudhi,” Sarah akaongeza.

Kwa sasa Sarah na Nasib wamesalia kuwa marafiki wakubwa, mrembo huyo akiwa tayari ana familia yake.