Habari

Sarah Wairimu kujua hatima ya wakili wake Alhamisi

October 1st, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI na SAM KIPLAGAT

SARAH Wairimu Kamotho ambaye ni mshukiwa wa mauaji ya bwanyenye Tob Cohen, atajua hatima yake Alhamisi korti itakapoamua iwapo wakili wake Philip Murgor ni kiongozi wa mashtaka au la.

Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) ameambia mahakama kuu Jumanne kwamba kuteuliwa kwa Philip Murgor kuwa kiongozi wa mashtaka hakujatenguliwa.

“Tungali kwenye mchakato wa kutengua kuteuliwa kwake,” naibu DPP Catherine Mwaniki amemuambia Jaji Stella Mutuku.

Kwa upande wake Murgor amesema jinsi ambavyo Kamotho ameshughulikiwa na vyombo vya dola ni sawa na kufungwa hata kabla ya kupandishwa kizimbani na kufunguliwa mashtaka.

“Ni suala la uzito sana ikizingatiwa kwamba huyu ni raia ambaye amekuwa akizuiliwa yumkini siku 35,” amesema Murgor.

Murgor amesema alijiuzulu kuwa kiongozi wa mashtaka Machi 7.

Aidha, amewasilisha barua aliomwandikia DPP Noordin Haji, akijiuzulu mara moja. Amesema aliacha kuwa kiongozi wa mashtaka wakati huo.

Amesema ombi lake lilikubalika na DPP mwenyewe.

Mahakama sasa itatoa uamuzi wake Alhamisi.