Habari Mseto

Sarakasi ndani ya serikali ya Jubilee waziri akimsema Ruto kwa wadogo walio katika DCI

June 28th, 2019 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

MWISHONI mwa Mei akiwa katika mahojiano na kituo cha redio cha Kameme, Naibu Rais William Ruto aliulizwa ikiwa alikuwa na habari kuwa ndani ya vitengo vya usalama kulikuwa na maafisa ambao walikuwa wakimdharau.

Swali hilo lilijikita kwa msingi kwamba katika hafla kadhaa za Ruto mashinani, kuna maafisa wa usalama ambao walikuwa wakimsusia hivyo basi kumwangazia kama aliyekuwa hatambuliwi na vitengo hivyo.

Kwa mafumbo, Ruto alijibu: “Mimi ni Naibu Rais wala sio mpikaji chai au askari rungu ndani ya serikali na nitashughulika nao. Idara za usalama ni kama soko kubwa ambako ndani yake kuna baadhi yao ambao ni wazembe, wajinga na wapuuzi.”

Wandani wa Ruto walikuwa wamemtambua katibu maalumu katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Karanja Kibicho kama aliyekuwa akiwaelekeza maafisa hao wasusie hafla zake mashinani.

Kwa upande wake, Kibicho alishikilia kuwa Ruto alikuwa na mazoea ya kuzuru mashinani bila mpangilio wowote wa kiusalama na ambapo alihitajika kutoa ratiba yake ya ziara mashinani kwa wizara hiyo ili mikakati ya kiusalama iwekwe.

“Usalama wa Naibu Rais unaanza naye binafsi. Atusaidie kumlinda ndio tumlinde,” akasema Kibicho.

Ni vita hivi vya kimaneno ambavyo vimechacha kiasi kwamba Kibicho amelalamika kwa idara ya uchunguzi wa Jinai kwamba Ruto anamhangaisha.

Kwa mujibu wa wakili Godfrey Kahuthu wa mahakama kuu, kuhangaishwa katika ajira sio suala la uchunguzi wa jinai bali ni la kuwasilishwa kwa wakuu wa vitengo ili kamati husika ndani ya ajira ziwajibikie maridhiano.

“Kibicho hajasema kuwa alipigwa na Ruto, akatukanwa, akatishiwa maisha au akaibiwa mali yake na Ruto bali anateta kuwa Ruto kama mkubwa wake hampi amani katika huduma ya serikali. Anateta kuwa Ruto ni kama hamtambui akiwa katibu maalumu… Huu ni sawa na ujinga ndani ya serikali hii,” anasema Kahuthu.

Bw Kahuthu anasema sarakasi kuu ni Kibicho ambaye ni mdogo wa Ruto kikazi serikalini amekimbia kumshtaki kwa wadogo wao wote ambao ni maafisa wa polisi katika DCI.

Bw Kahuthu anatafakari: “Kwani Rais Uhuru Kenyatta amezima wanaohudumu katika serikali yake kumpa malalamishi ya kikazi ndipo Kibicho akimbie kushtaki Naibu Rais kwa DCI?”

Anauliza kwani ndani ya serikali hii haina mpangilio wa maridhiano ndio migongano ya mawaziri na maafisa wengine wakuu iwe ya kuanikwa hadharani?

“Lakini hakuna lisilo la kawaida hapa kwa kuwa hata Rais huobnekana hadharani akiteta vikali na kwa hisia hasi na hasira badala ya kuwapa wadogo wake mialiko ya kinidhamu…Lakini hali hii sasa imegeuza serikali kuwa mnara wa babeli ambapo hakuna anayemsikiza mwingine, heshima na nidhamu zikiwaadimikia maafisa wa serikali hii kwa kiwango kikuu,” anasema Bw Kahuthu.

Kibicho achunguzwe

Hayo yakijiri, naye mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua amependekeza Bw Kibicho achunguzwe kuhusu baadhi ya amri zake kwa wadogo wake nyanjani.

Amesema kuwa Kibicho amekuwa akiwaagiza makamishna na makamanda wa vitengo vya usalama mashinani kutohudhuria hafla za Ruto.

Gachagua ambaye pia alikuwa afisa wa utawala wa kimaeneo katika serikali ya Rais Mstaafu Daniel Moi kabla ya kujiuzulu kujiunga na siasa alisema kuwa wanaowekwa katika hatari ya kikazi ni maafisa hao ambao wanashawishika kutoheshimu Dkt Ruto.

“Ikiwa huyu Dkt Ruto ataibuka kuwa Rais baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, maafisa hawa watategemea nini kutoka kwa huyu wanayeonyesha dharau akiwa Naibu Rais?” akahoji.

Akasema: ‘Tumeshuhudia hali kadhaa ikiwemo katika Kaunti yangu ya Nyeri ambapo kumezuka uchochezi wa kiafisi kwa baadhi ya maafisa wa kiusalama nyanjani wasihudhurie hafla ya rais. Tunataka kujua jinsi amri hizi hutolewa.”

Bw Gachagua alisema Katiba ya nchi imezima maelekezi ya maamuzi kwa masuala ya kikatiba kupokezanwa kutoka kwa wakubwa hadi kwa wadogo kupitia simu au neno la mdomo.

“Maamuzi ya aina hiyo yanafaa kuwekwa katika barua rasmi na itiwe sahihi na anayeitoa kwa manufaa ya msasa kuhusu uhalali wa amri hizo,” akasema.

Alisema wakishindwa kujieleza ni kwa nini wanafanya hivyo “bila shaka watajua kuna sheria ya kufuatwa.”

Alisema Naibu Rais akitembelea eneo la hapa nchini hafanyi hivyo kama mtu binafsi bali hufanya hivyo kama Naibu Rais na ambaye hafla zake ni za kitaifa katika mikakati ya kuziandaa.

“Tunapouliza kisiri, tunaarifiwa kuwa Kibicho ndiye ametoa amri hizo. Ajue kuwa sisi tuko na uhuru bungeni wa kumumulika. Asifikirie kuwa tunanyamaza kwa upole wa uoga…Hapana, chuma chake ki motoni,” akasema.

Na hayo ndiyo mahangaiko ya Bw Kibicho ambayo anataka DCI ichunguze, wengine pembeni wakihofia kuhusu kauli ya wahenga kuwa njia ya mhini na mhiniwa huwa ni moja.