Habari

SARAKASI ZA KCPE: Karatasi zatoweka, mtahiniwa na wazazi ndani

November 1st, 2018 2 min read

Na WAANDISHI WETU

VIMBWANGA vilishuhudiwa kutoka kwa walimu, watahiniwa, wazazi na maafisa kwenye siku ya pili ya mtihani wa darasa la nane (KCPE) katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Katika shule ya Oloonamuka, Kaunti ya Narok, karatasi za mitihani ya Kiswahili na Sayansi zilitoweka kabla ya kufikishwa shuleni, hali iliyozua taharuki miongoni mwa watahiniwa na wazazi.

Ilibidi maafisa waliosimamia shughuli hiyo kuomba karatasi kutoka shule jirani ndiposa wakafanya nakala zilizotumika na watahiniwa hao, baada ya kushauriana na Baraza la Mitihani (KNEC)

Ilibidi Kamishna wa Kaunti ya Narok, Bw George Natembeya kuongoza operesheni ya kutafuta karatasi hizo, ambapo baadaye watu 11 akiwemo mwalimu mkuu wa shule hiyo na maafisa watatu wa usalama walikamatwa.

Katika Kaunti ya Kisii, watu watano akiwemo mwanafunzi wa miaka 14 wa kidato cha kwanza, mama yake na babake walitiwa mbaroni na kufikishwa katika mahakama ya Ogembo ambako walishtakiwa kwa kujifanya watahiniwa kwa nia ya kudanganya katika mtihani huo.

Mwanafunzi huyo alipatikana akifanya mtihani wa KCPE katika shule ya msingi ya Eburi, kaunti ndogo ya Nyamache na maafisa wa polisi ambao walikuwa wakilinda mtihani.

Polisi walisema mwanafunzi huyo wa shule ya upili ya Nyabonge alikuwa amesajiliwa kama mtahiniwa katika shule ya kibinafsi ya Scania Academy na wazazi wake bila ufahamu wake.

Mwanafunzi huyo, wazazi wake Reuben Mogaka na Eunice Magoma pamoja na George Mosota Nyanga’u, Nyamwamu na Mark Mogaka Maobe walifikishwa kortini ambapo mahakama iliagiza wazuiliwe rumande hadi uchunguzi ukamilike.

Katika Kaunti ya Nyandarua, mwalimu mkuu alikamatwa kwa kwenda kuchukua karatasi za mtihani akiwa mlevi chakari jana alfajiri. Bw Peter Kamau Ndegwa alikamatwa alipofika katika ofisi za Kamishna wa Kaunti mjini Ol kalou akipiga kelele na kutembea kwa shida kwa sababu ya ulevi.

Alikiri shtaka mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi wa Nyahururu, Ocharo Momanyi na kuzuiliwa rumande hadi Jumanne wiki ijayo ripoti kuhusu tabia yake itakapowasilishwa kortini kabla ya kuhukumiwa.

Eneo la Pwani, wanafunzi wawili eneo la Magarini, Kaunti ya Kilifi walikosa kufanya mtihani baada ya kuolewa. Naibu Kamishna Simon Lokorio alisema watahiniwa hao kutoka shule ya msingi ya Kaembeni waliolewa vijiji vilivyo karibu.

Katika Kaunti ya Kwale, mtahiniwa alijifungua mtoto wa kike jana asubuhi. Msichana huyo mwenye umri wa miaka 19, ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya Tswaka eneobunge Lunga Lunga.

Kamishna wa Kaunti ya Kwale, Bw Karuku Ngumo alisema msichana huyo alihamishwa hadi zahanati ya Tswaka ambako alifanyia mtihani.

Katika Kaunti ya Embu, watahiniwa wawili wanafanyia mtihani wakiwa hospitali baada ya mmoja kupata mtoto na mwingine kuvunjika mguu.

Msichana mwenye umri wa miaka 13 katika shule ya msingi ya Mwanyani, Mbeere Kusini alipata maumivu ya kujifungua na kukimbizwa hospitali ya Kiritiri Level Four.

Katika eneo la Butere, Kaunti ya Kakamega, msichana mwingine alifanya mtihani akiwa hospitali baada ya kujifungua. Mkuu wa elimu eneo la Butere, Bw Martin Likoko alisema mipango ilikuwa imefanywa ili aweze kufanyia mtihani huo hospitalini.

Na Benson Matheka, George Sayagie, Jadson Gichana, Charles Wanyoro, Benson Amadala, Fadhili Fredrick, Samuel Baya, Charles Lwanga na Ahmed Mohamed