SHINA LA UHAI: Saratani ya mifupa inayolemaza waathiriwa

SHINA LA UHAI: Saratani ya mifupa inayolemaza waathiriwa

Na PAULINE ONGAJI

KWA takriban miaka 15, Esther Nyambura Gitau, 39, mkazi wa Kaunti ya Kiambu alipambana na maradhi ya kansa ya mifupa.

Na japo ni vita ambavyo kwa sasa kulingana na madaktari amevishinda, maradhi haya yalimsababisha kukatwa sio tu mkono wake wa kulia, bali pia bega lake la kulia liliondolewa lote.

Bi Gitau aligundulika kuwa na kansa ya mifupa aina ya chondrosarcoma mwaka wa 2007. Tatizo lake lilianza kama maumivu makali kwenye mkono wake wa kulia.

Anasema kwamba madaktari hawakuwa na uhakika nini hasa kilichosababisha shida hii.

“Awali nilikuwa nimejeruhiwa nikifanya kazi katika kiwanda kimoja, lakini nilipuuza maumivu ya mwanzoni na badala ya kufanyiwa uchunguzi wa kina wa kimatibabu, nilikuwa nameza na kujipaka dawa za maumivu,” aeleza.

Kwa miaka saba alifanyiwa chunguzi nne za seli na tishu (biopsy) kabla ya kuruhusiwa kupokea matibabu ya aina yoyote ile.

Lakini maumivu haya yalizidi mwaka wa 2014 ambapo baada ya chunguzi kadhaa, alianza matibabu ya tibaredio mapema mwaka huo.

Hata hivyo baada ya miezi mitano, daktari alimshauri kwamba ili kupata nafuu na suluhu ya kudumu, sharti mkono huo ungeondolewa.

Mwanzoni alikataa katakata kumsikiza daktari kwani hakuona jinsi angeendelea kuishi bila sehemu hii ya mwili.

“Wakati huo nilikuwa nimejifungua mtoto wangu wa kwanza, kwa hivyo nilikumbwa na ugumu kwani nilikuwa mama mchanga na bado nilikuwa napambana na maradhi ambayo hayakuwa yakieleweka,” aeleza.

Hata hivyo, maumivu yalipozidi mwezi Mei mwaka wa 2014, alisalimu amri. “Kumbuka kwamba nilikuwa nimepoteza uwezo wa kutumia mkono huo mwaka mmoja awali, kutokana na maumivu makali. Mkono huo ulikuwa umevimba na ulikuwa unatoa majimaji yenye harufu mbaya. Ni hapo niliamua kwamba wakati umewadia wa kukubaliana na uamuzi wa daktari,” asema

Baada ya upasuaji huo, ilimchukua muda kujifunza kuishi bila mkono wake na kujifanyia mambo ya kawaida na hatimaye akazoea.

Lakini hata kabla ya kupona kabisa na kuzoea maisha yake mapya, janga likarejea. Huu ulikuwa mwaka wa 2019 ambapo Bi Gitau alianza kukumbwa tena na maumivu. Baada ya kurejea hospitalini na kufanyiwa uchunguzi, iligundulika kwamba kansa ilikuwa imerudi.

“Wakati huu bega la upande wa kulia lilikuwa limeathirika. Ili kudhibiti hali hii, daktari aliamua nifanyiwe upasuaji mwingine wa kuondoa bega lote, matibabu yaliyoambatanishwa na awamu 30 za tibaredio,” aeleza.

Kwa sasa ni mwaka mmoja tangu athibitishwe kwamba amepona kansa hii. Bila shaka hii ni nafuu kwa familia hii, lakini haijakuwa rahisi.

Kando na unyanyapaa na udhaifu unaoambatana na matibabu ya maradhi haya, mzigo mkubwa umekuwa ule wa fedha za kugharimia matibabu haya. “Kufikia kiwango cha kuondolewa mkono na bega, vilevile jumla ya awamu 55 za tibaredio, tumetumia zaidi ya Sh5M kwa matibabu.

Bi Gitau ana bahati kwani wakati huo wote mumewe ambaye amafanya kazi ughaibuni, aliweza kugharimia matibabu yake. “Aidha, pamoja na usaidizi wa marafiki hasa kansa iliporejea mara ya pili, mzigo wa gharama ya matibabu haukumlemea sana,” aongeza.

Kulingana na wataalam, kansa ya mifupa ni nadra sana ambapo inajumuisha asilimia moja pekee ya kansa zote zilizokithiri.

Dkt Brian K. Rono, daktari wa mifupa na mtaalam wa upasuaji wa majeraha jijini Nairobi, asema kansa ya mifupa yaweza anza katika mfupa wowote kwenye mwili, lakini mara nyingi huathiri fupanyonga au mifupa mirefu ya mikono na miguu.

Kwa upande mwingine, chondrosarcoma ni mojawapo ya aina za kansa za mifupa na huathiri mifupa na viungo vya mwili. “Aidha, chondrosarcoma ni nadra miongoni mwa aina za kansa za mifupa zilizokithiri huku ikiwakilisha asilimia 20 pekee. Katika aina hii ya uvimbe, seli za kansa husababisha gegedu (cartilage) na mara nyingi hutokea kwenye nyonga, miguu,au mkono hasa miongoni mwa watu walio katika umri wa makamo na waliozeeka,” aeleza.

Dkt Rono anasema ishara za kansa ya mifupa ni pamoja na maumivu na uvimbe karibu na sehemu iliyoathirika. “Pia mfupa ulioathirika hudhoofika na hata kuvunjika, huku mwathiriwa akikumbwa na uchovu wa kila mara na hata kupoteza uzani,” asema.

Chanzo

Kulingana na wataalam, kansa hii hutokana na mambo kadha wa kadha, ikiwa ni pamoja na hitilafu za jeni zinazopitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, kama vile Li-Fraumeni Syndrome na Hereditary Retinoblastoma.

Aidha, ugonjwa huu waweza tokana na maradhi ya mifupa yanayofahamika kama Paget’s Disease of Bone, ambayo huwakumba hasa watu wazee.

“Aidha, maradhi haya yaweza tokana na matatizo ya kiafya kutokana na matibabu ya awali ya tibaredio,” aeleza .

Mbali na hayo, wataalam wanahoji kwamba yaweza tokana na kupona kwa jeraha kusiko kwa kawaida.

Kwa mujibu wa Dkt Rono, inaweza pia kusababishwa na aina zingine za kansa zilizosambaa hadi kwenye mifupa. “Lakini kwa kawaida, kansa ikianzia sehemu zingine mwilini na kuenea kwenye mifupa, haitatambulika kama kansa ya mifupa. Itadumisha jina halisi ya sehemu ambapo ilianzia,” aeleza.

Anasema aghalabu tiba itategemea awamu ya maradhi haya. Hata hivyo mara nyingi tiba itahusisha upasuaji kuondoa sehemu ya mfupa ulioathirika.

“Inawezekana kuunda upya au kubadilisha mfupa uliondolewa, lakini mara nyingi sehemu iliyoathirika lazima iondolewe. Aidha, hutibiwa kupitia tibakemia inayohusisha kuangamiza seli za kansa kwa kutumia dawa yenye nguvu, na tibaredio ambapo miyale inatumika kunywea seli za kansa,” aongeza.

Lakini anasema kuna baadhi ya uvimbe usio wa kansa ambao hutokomea pasipo tiba.

You can share this post!

Leads United inapigiwa chapuo kufanya kweli

Uhuru achoshwa na hotuba yake mwenyewe

T L