Michezo

Sare kwa Sharps Boys na Volcano FC, Kinyago yainyeshea Locomotive 4-0

August 28th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Sharps Boys na Volcano FC kila moja iliyeyusha pointi mbili muhimu huku Kinyago United ikivuna magoli 4-0 mbele ya Locomotive FC kwenye mechi za Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 14 iliyosakatiwa uwanjani KYSD, Kamukunji Nairobi.

Mohamed Ali alifungia Sharp Boys huku Volcano FC ikisawazisha kupitia Victor Mugambi na kumaliza ubishi wa nani mkali.

Mabingwa wa taji hilo Kinyago United iliingia mzigoni ikilenga kutesa na kunasa alama tatu muhimu ili kujiongezea matumaini ya kufanya kweli msimu huu.

Chipukizi hao walinasa ushindi huo kupitia Henry Thiery aliyepiga ‘Hat trick’ naye nahodha wake, Samuel Ndonye aliitingia goli moja.

Kocha wa Lehmans, Abdulrahman Ali akishaurina na wachezaji wake tayari kukabili Pro Soccer Academy kwenye mechi za Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 14, ugani KYSD Kamukunji, Nairobi. Lehmans ilizoa ushindi wa mezani baada ya wapinzani kuingia mitini. Picha/ John Kimwere

”Tulikubali yaishe raundi hii lakini wapinzani wetu watarajie kivumbi kikali kwenye mechi za mkumbo wa pili,” kocha wa Sharp Boys, Boniface Kyalo alisema.

Kufuatia matokeo hao, Kinyago ingali kifua mbele kwa alama 18, nne mbele ya Sharp Boys baada ya kusakata mechi sita na saba mtawalia.

Nayo Tico Raiders ilizabwa mabao 2-1 na Young Achievers wakati Lehmans FC ilituzwa pointi tatu bila jasho ikiwa ni ushindi wa mezani baada ya wapinzani wao Pro Soccer Academy kuingia mitini.

Magoli ya Young Achievers yalifumwa kimiani na Giovan Clinton naye Brain Opiyo alitingia Tico Raiders bao la kufuta machozi. Kwenye matokeo hayo, Pumwani Ajax iliilaza Pumwani Foundation mabao 2-0, Gravo Legends ilirarua Young Elephant kwa magoli 5-1, Fearless FC ililimwa mabao 2-0 na MASA nayo Fearless Academy ilitoka nguvu sawa bao 1-1 na State Rangers.