Habari

Sare mpya za polisi zitashonwa na NYS – Matiang'i

December 18th, 2018 2 min read

Na PETER MBURU

SERIKALI imeshikilia kuwa haitanunua tena sare za polisi kutoka nje ya nchi, ikisema kuwa kuna baadhi ya wakora ambao wamekuwa wakitumia nafasi hiyo kupanga njama za kula pesa za umma, badala ya kuinua viwanda vya humu nchini.

Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiangi Jumanne alisema kuwa kuna wakora wanaoisukuma serikali kununua sare za polisi kutoka mataifa ya nje, akisema ni watu hao ambao wamekuwa wakila pesa za umma kwa miaka mingi, badala ya kuinua viwanda vya humu nchini.

Dkt Matiangi alisema kuwa kwa sasa Shirika la Huduma kwa Vijana (NYS) linaendelea kutengeneza sare mpya ambazo polisi watatumia, akiongeza kuwa viwanda vya kutengeneza nguo kama Rivertext na vingine aidha vitapewa tenda hizo.

“Inspekta Jenerali, Katibu wa wizara name tumekuwa tukisukumwa na baadhi ya wakora na wezi tununue sare kutoka nje ya nchi. Nisikizeni kwa makini, hatutanunua sare za polisi kutoka nchi nyingine.

“Sasa wewe na wakora wako, mahali mlikubaliana mtaenda kununua sare utaenda uwaeleze hivi, hatutaenda kununua sare popote pengine. Ni rahisi hivyo tu,” akasema waziri huyo.

Mwakilishi Mwakilishi wa Homa Bay Bi Gladys Wanga asema na Mkuu wa Polisi Joseph Boinnet (kati) Mkuu wa Trafiki Samuel Kimaru katika makao makuu ya KICD, Nairobi Desemba 18, 2018. Picha/ Peter Mburu

Waziri huyo ambaye alikuwa akizungumza katika makao ya KICD jijini Nairobi alisema tayari viwanda vya humu nchini vimelipwa na serikali ili kutengeneza sare, baada ya timu kutoka wizara yake kuzuru viwanda vya nguo Eldoret, Nakuru na katika shirika la NYS.

Waziri huyo alisisitiza kuwa viwanda vya Kenya vina uwezo wa kutengeneza sare hizo, hivyo akiutaja kuwa ‘ujinga’ kuitaka nchi kununua sare kutoka nchi nyingine.

“Sharti tuinue viwanda vya nguo vya humu nchini. Tutasaidiaje wakulima wa pamba na watengenezaji katika viwanda na kuongeza nafasi za ajira bila kufanya hivyo. Kumekuwa na biashara ya gizani ambapo watu wanenda mahali na kuelewana kununua sare kutoka nje ya nchi, kisha kutoa vijisababu kuwa viwanda vyetu havina uwezo,” akasema Dkt Matiangi.

Alisema licha ya kuwa kenya ina uwezo wa kujitengenezea sare hizo, kuna baadhi ya watu wanaojaribu kueneza uvumi kuwa hilo haliwezekani.

“Itakuwa na haja gani kwa serikali kuweka pesa kuvumbua kiwanda cha Rivertext ili kutoa nafasi za kazi Eldoret kisha kesho yake kama wajinga twende kununua sare za polisi kutoka nje Uturuki, China ama pengine,” akauliza waziri huyo.