Michezo

Sare ya 2-2 dhidi ya Nakumatt yatamausha mashabiki wa Ingwe

May 13th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MASHABIKI wa AFC Leopards hawana raha kabisa baada ya timu yao kukabwa 2-2 na Nakumatt na kumaliza mechi ya nane bila ushindi kwenye Ligi Kuu uwanjani Kenyatta mjini Machakos, Jumamosi.

Wakizungumzia matokeo ya mchuano huu ambao Ingwe iliongoza 2-0 kupitia kiungo Whyvonne Isuza kabla ya kuruhusu Nakumatt kusawazisha kupitia Eugene Ambulwa na Brian Nyakan dakika 15 za mwisho, mashabiki wamesema wachezaji hawana ari kabisa.

“Huu ni mzaha. Njia ambayo timu ilitupa uongozi inatuwacha na maswali mengi. Hawa wachezaji wana ari kweli? Wanalenga kutimiza malengo gani kutokana na matokeo?” Nixon Mahasi alichemka.

Kamwaro Kamwaro pia alielekeza lawama kwa wachezaji. “Niliposema kocha hawezi kupata ushindi ikiwa wachezaji hawajitolei, watu walisema nina kiburi. Hadi wale waliofukuza (kocha Robert) Matano waondoke, utovu wa nidhamu bado utasalia. Hapa hakuna timu,” alisema.

Maggy Asiko alitaka mashabiki wenzake kugoma kuhudhuria mechi za Ingwe akisema wachezaji “wanachezea hisia zetu”.

Mashabiki wengi wamesikitishwa na matokeo haya. Baadhi yao wametaja kocha mpya Rodolfo Zapata kama ‘mtalii anayestahili kutimuliwa’, huku sehemu kubwa ikionekana kutaka Matano, ambaye aliachishwa kazi kighafla miezi michache iliyopita, arejeshwe. Hata hivyo, Matano anaendelea kufanya vyema katika klabu yake mpya ya Tusker baada ya kushinda mechi tatu zilizopita kwa kulaza Wazito 1-0, SoNy Sugar 3-2 na Bandari 2-0. Tusker itapiga mechi yake ya 15 hapo Jumapili dhidi ya Kariobangi Sharks.

Mechi kati ya Mathare United na Bandari iliyotanguliwa kusakatwa uwanjani Kenyatta ilimalizika bila mshindi, 0-0.

Sofapaka ilikuwa na siku nzuri mjini Narok baada ya kutoka chini bao moja na kulipua Zoo Kericho 2-1. Mwanasoka bora wa Kenya mwaka 2017, Michael Madoya aliweka Zoo mbele dakika ya 12. Humphrey Okoti alisawazisha dakika tano baadaye kabla ya Stephen Waruru kuongeza bao la ushindi dakika ya 53.