Michezo

Sare ya Atalanta shubiri kwa Juve

July 25th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

ATALANTA walidumisha uhai wa matumaini finyu ya kuwapiga Juventus katika hatua za mwishomwisho za kampeni za msimu huu na kunyanyua Ligi Kuu ya Italia (Serie A) baada ya kuwalazimishia AC Milan sare ya 1-1 mnamo Julai 24, 2020.

Hakan Calhanoglu aliwaweka wenyeji AC Milan kifua mbele uwanjani San Siro kupitia mpira wa ikabu katika dakika ya 14.

Hata hivyo, wageni Atalanta walirejeshwa mchezoni na Duvan Zapata aliyesawazisha mambo kunako dakika ya 34. Bao hilo lilikuwa la 18 kwa kiungo mvamizi raia wa Colombia.

Matokeo hayo yanamaanisha kwamba Atalanta kwa sasa wanajivunia alama 75, tano nyuma ya viongozi Juventus ambao wana mchuano mmoja zaidi wa kusakata ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimetandazwa na washindani wao wakuu.

Atalanta ambao pia wanafukuzia ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kadri wanavyojizatiti kuchuana na Paris Saint-Germain (PSG) katika robo-fainali.

Chini ya kocha wa zamani wa Chelsea, Maurizio Sarri, Juventus huenda wakajitwalia ubingwa wa Serie A kwa msimu wa tisa mfululizo iwapo watawaangusha Sampdoria mnamo Julai 26, 2020.