Michezo

Sarri akiona kusema Kante hawezi kucheza 'Sarri ball'

April 17th, 2019 1 min read

NA JOHN ASHIHUNDU

LONDON

Mashabiki wa Chelsea wamemshutumu vikali kocha wao, Maurizio Sarri kufuatia madai yake kwamba kiungo N’Golo Kante hawezi kucheza soka ya kugonga pasi moja moja almaarufu ‘Sarri ball’.

Kante amekuwa kipindi cha idadi kubwa ya mashabiki wa Chelsea tangu atue Stamford mnamo 2016 akitokea Leicester City.

Kabla ya ujio wa Sarri, Mfaransa huyo alikuwa akicheza kama kiungo wa katikati, lakini sasa anachezeshwa kama kiungo mshambuliaji.

Sarri ameamua kumpa Jorginho nafasi hiyo huku akidai kwamba Muitalaini huyo amemshinda Kante kwa ufundi.

“Kucheza katikati lazima uwe mtu anayeweza kuamua mambo kwa haraka na kugusa mpira mara moja kwa haraka,” alisema kocha huyo mwenye umri wa miaka 60.

Lakini madai ya mkufunzi huyo yameibua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wa Chelsea ambao wamesema hawakubaliani ni madai hayo.

Wengi wamesisitiza hawawezi kumuunga mkono kuhusu madai hayo, hata kama anaifanya timu hiyo ishinde taji.