Michezo

Sarri amsikitikia Klopp kwa kukosa taji EPL

May 13th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MENEJA wa Klabu ya Chelsea Maurizio Sarri amemhurumia mwenzake wa Liverpool Jurgen Klopp baada ya Mjerumani huyo kukosa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza(EPL).

Liverpool walipigwa kumbo kwenye kiny’ang’anyiro cha kutwaa EPL Jumapil Mei 12 baada ya Manachester City kuichapa Brighton 4-1 na kufikikisha jumla ya alama 98. Ushindi wa 2-0 wa The Reds dhidi ya Wolvehampton uliwawezesha kufikisha alama 97 huku bingwa mpya akipatikana siku hiyo ya mwisho ya ligi.

Akizungumza baada ya Chelsea kukabwa 0-0 ugenini na Leicester, Sarri alisema Klopp alipitia uchungu sana kuona taji likimponyoka pembamba licha ya kuwa kileleni mwa jedwali kwa majuma kadhaa.

Sarri alipitia hali kama ya Klopp kwenye msimu wake wa mwisho akiifunza Napoli katika ligi ya Serie A aliposhindwa pembamba na Juventus licha ya kufikisha alama 91.

“Naelewa uchungu wa mwenzangu Klopp. Ni ngumu kuamini kwamba unaweza kufikisha alama 97 kwenye ligi lakini ukakosa kuishinda. Liverpool imekuwa na msimu wa kuridhisha na kukosa kutwaa ubingwa wa EPL ni chungu na vigumu kuelewa,

“Nilikumbana hali hiyo nikiifunza Napoli kwenye Ligi ya Italia(Serie A) wakati tulifikisha alama 91 lakini kombe likabebwa na wapinzani wetu Juventus. Kwa hivyo naelewa sana uchungu wake,” akasema Sarri