Michezo

Sarri amtetea Jorginho baada ya kuzomewa na mashabiki

March 13th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MKUFUNZI wa Chelsea FC Maurizio Sarri amemtetea kiungo Jorginho aliyezomewa na baadhi ya mashabiki ugani Stamford Bridge wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza dhidi ya Wolvehampton Wanderers Jumapili Machi 10, 2019.

Mashabiki wa Chelsea maarufu kama The Blues wamekuwa wakishmtumu Jorginho kutokana na kiwango cha chini cha mchezo wake na walidhihirisha hilo wazi, raia huyo wa Italia alipondolewa uwanjani dakika ya 72 ili kumpisha Willian, katika mechi ambayo Chelsea walihitaji bao la dakika ya mwisho kusajili sare ya 1-1 nyumbani.

Wolves walitangulia kufunga kupitia Raul Jiminez dakika ya 56 huku Eden Hazard akikomboa bao hilo dakika ya 92 katika muda wa ziada.

Ingawa hivyo, Sarri amemtaka Jorginho kujipa moyo na kujifunza kuhimili presha kutoka kwa mashabiki huku akisema anapitia mtihani huo kutokana na umuhimu wake kikosini.

“Jorginho huwa yupo matatani iwapo wachezaji wengine wanakosa kuzifikia pasi zake. Huwa yupo tayari kumega pasi mara moja lakini hilo linamwia vigumu iwapo wachezaji wengine hawasongi mbele kupokea mipira yake,”

“Vile vile mtindo wa uchezaji wa 4-2-3-1 haumfai kabisa haswa mechi ikielekea kukamilika. Namfahamu vizuri kwasababu nimefunza soka kwingine yeye huingia matatani wachezaji wenzake wakikosa kusonga mbele kupokea pasi zake. Hata hivyo ana nidhamu ya juu ndani na nje ya uwanja,” akasema Sarri.