Michezo

Sarri awapa Chelsea malengo ya kutwaa ubingwa wa Uropa

March 27th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

KOCHA wa Chelsea, Maurizio Sarri amesema itabidi klabu hiyo ishinde ubingwa wa Europa League ili ijihakikishie nafasi ya kucheza katika michuano ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Hii ni baada ya timu hiyo ya Stamford Bridge kushindwa 2-0 na Everton, matokeo ambayo kocha huyo aliyaona huenda ndicho kikomo kwa vijana wake kuwania nafasi ya nne-bora kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Sarri alisema timu yake ilicheza vizuri katika kipindi cha kwanza, lakini ikashindwa kufunga mabao, mbali na kushindwa kufikiria zaidi katika kipindi cha pili kwenye mechi hiyo iliyochezewa Goodison Park.

Kocha huyo alisema haikuwa mara ya kwanza kushuhudia mchezo wa aina hiyo kutoka kwa vijana wake, msimu huu.

Kichapo hicho kimeiacha Chelsea katika nambari ya sita ligini, pointi tatu nyuma ya Arsenal walio katika nafasi ya nne na kuzua maswali magumu miongoni mwa mashabiki waliofikiria Sarri ndiye angewaondoa katika matatizo yao kwa sasa.

“Iwapo tutaendelea kucheza kama tulivyocheza dhidi ya Everton katika kipindi cha pili, tutajipata katika nafasi mbaya jedwalini,” alisema Sarri.

Kwenye mechi hiyo, staa Eden Hazard aligonga mwamba wa goli huku Ross Barkley aking’ara katika safu ya kati, licha ya foka za mashabiki wa Everton, klabu yake ya zamani.

Kocha afoka

Kocha Sarri amekuwa akiwakosoa wachezaji wake vikali msimu huu, akimfokea Hazard, licha ya nyota huyo kuwa na asilimia 48 ya mabao ya klabuni humo msimu huu.

Kocha huyo majuzi alishangaza ulimwengu aliposema kuwa huenda akafutwa kazi kutokana na matokeo mabaya yanayoiandama timu hiyo.

Lakini huenda akaponea iwapo ataisaidia kutwaa ubingwa wa Europa League, ushindi ambao utawapa njia ya mkato kufuzu kwa michuano ya Klabu Bingwa barani Ulaya.

Sarri anatarajiwa kumaliza msimu huu na baadaye aongeze wachezaji wazuri kadhaa ambao watasaidia Chelsea kuzuia kushindwa katika mechi ngumu msimu ujao.

Hata hivyo, kuna vikwazo vikubwa kwa jambo kama hilo kufanyika kufuatia vikwazo vya marufuku dhidi ya klabu hiyo kununua wachezaji wapya hadi 2020, uamuzi ambao klabu hiyo inajaribu kukata rufaa.

Hali hiyo inachochewa zaidi na uvumi kwamba huenda wachezaji kadhaa, akiwemo Hazard wakaondoka.

Hazard anatarajiwa kuyoyomea Real Madrid, wakati Callum Hudson-Odoi akizidi kuwindwa na Bayern Munich ambayo tayari imewasilisha ombi.

Alipoulizwa iwapo ana wasiwasi kuhusu matumaini ya timu yake kuwepo katika nafasi ya timu nne bora, alisema: “Iwapo tutacheza vile tulivyocheza katika kipindi cha pili, hatutafulu.”