Habari

Sasa serikali yamtetea Passaris

June 8th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia Margaret Kobia amemshutumu Gavana wa Nairobi Mike Sonko kwa kumkosea heshima Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Esther Passaris wakati ya sherehe za Madaraka Dei.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Profesa Kobia alisema amekerwa zaidi na mtindo mbaya unaoendelea ambapo wanawake wanaoshikilia nyadhifa za uongozi hudhalilishwa hadharani.

Waziri huyo ambaye anasimamia masuala ya usawa wa kijinsia na mipango ya kuimarisha maisha ya wanawake, aliungana na wanawake wengine kumtetea Passaris, akisema wanawake viongozi hawapaswi kushambuliwa kwa maneno ya kudunisha katika maeneo ya hadhara.

“Hatua ya Gavana Sonko kumshambulia Bi Passaris, kwa maneno ya kudunisha hadharani wakati wa sherehe ya Madaraka Dei ni dhuluma ya kijinsia. Ni mfano mbaya machoni pa watoto,” Profesa Kobia akasema.

“Viongozi wanapaswa kujidhibiti hata kama wamekosewa. Sio vizuri kwa kiongozi kumrushia mwenzake maneno ya kuaibisha jinsi hivyo hadharani,” akaongeza.

Profesa Kobia alitoa hakikisho kwamba wizara yake itaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha kuwa watu hawadhulumiwi au haki zao kuhujumiwa kwa misingi ya jinsia yao.

“Azma ya wizara yangu ni kuhakikisha kuwa Wakenya, waume kwa wake, wanapaswa kufanya kazi pamoja kuimarisha taifa hili,” akaeleza.

Miongoni mwa wanawake waliomtea Bi Passaris ni Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo aliyetumia jukwaa la bunge kumkashifu Gavana Sonko.

Mnamo Jumamosi, Bi Passaris aliondoka kwa hasira kutoka ukumbi palipoandaliwa sherehe za Madaraka Dei katika uwanja wa Pumwani baadhi ya kuelekezewa mishale ya maneno na Bw Sonko.

Lalama

Hii ni baada ya mbunge huyo kulalamika kuwa Gavana Sonko hupuuza simu zake anapotaka kuuliza kuhusu masuala muhimu kwa wakazi wa Nairobi.

“Unanipigia simu kwa nini? Mimi sio bwana (mume) yako!” akafoka Gavana Sonko.

Chama cha Mawakili Wanawake (FIDA) kimataka Bw Sonko akamatwe na kushtakiwa kwa kosa la kutumia lugha ya chuki dhidi ya Bi Passaris.

Shirika la Habari la Royal Media Jumatano lilizima kipindi cha JK Live kinachoongozwa na Jeff Koinange wakati Gavana Sonko alianza kujitetea kutokana na shutuma za Passaris. Gavana huyo alikuwa amealikwa kwa mahojiano kuhusu masuala mbalimbali yanayowahusu wakazi wa kaunti ya Nairobi.