Kimataifa

Saudi Arabia kufungua duka la pombe kwa mabalozi

January 25th, 2024 2 min read

NA MASHIRIKA

RIYADH, SAUDI ARABIA

SAUDI Arabia inajiandaa kufungua duka la pombe la kwanza jijini Riyadh kuhudumia mabalozi pekee ambao si Waislamu.

Haya ni kwa mujibu wa dokezo la anayefahamu mipango hii na stakabadhi ambayo shirika la Reuters liliona.

Wateja watahitajiwa kujisajili kupitia apu ya simu, wakaguliwe na wizara ya mashauri ya kigeni na kufuata vipimo vya kila mwezi wanaponunua vileo.

Ni badiliko la kihistoria katika ufalme huo ambao unalegeza itikadi ya kiislamu ili kupanua sekta ya utalii na uwekezaji sababu unywaji pombe ni marufuku.

Pia, ni mpango mpana wa azma ya 2030 kujenga mfumo wa uchumi usiotegemea mafuta pekee.

Duka hilo liko katika makao ya mabalozi Riyadh Diplomatic Quarter na litaruhusu wasio waislamu pekee.

Waraka huo haukuweka wazi iwapo wahamiaji ambao si waislamu na mabalozi wataruhusiwa humo.

Imebainika duka hili litafungulia majuma kadhaa yajayo.

Wanaokiuka kanuni na kunywa pombe Saudia hucharazwa mamia ya mijeledi, hurejeshwa nchini mwao, hutozwa faini ama kutupwa gerezani.

Wanywaji wamekuwa wakipata pombe kupitia njia za magendo na kupitia mabalozi.

Serikali ya Saudia ilithibitisha habari kuwa imeweka vizingiti vipya kwa uagizaji pombe kutoka mataifa mengine kupitia usafirishaji mizigo baina ya mabalozi.

Kituo cha Mawasiliano ya Kimataifa (CIC) ilisema kanuni hizi mpya zimetolewa ili kukabili biashara haramu ya bidhaa za pombe zinazopokelewa na misheni ya kibalozi.

CIC ilisema mfumo huu mpya wa kudhibiti biashara za ubalozi unaheshimu makubaliano ya mataifa yanayohusiana.

Kwa miongo mingi, Saudia imekuwa na sheria kali sana za kijamii.

Ila miaka ya hivi karibuni, imelegeza kanuni za kutangamana kama vile kutenganisha wanaume na wanawake katika maeneo ya umma na wanawake kutakiwa kuvaa mabuibui meusi ama mitandio.

Mwanamfalme Mohamed kugandia mamlaka kumefuatwa na mabadiliko ambayo yanahusisha ufunguzi wa nchi kwa utalii kwa wasio waislamu, matamasha na kuruhusu wanawake kuendesha magari.

Pia, msako na udhibiti wa wapinzani wa kisiasa umeanza kulegezwa.

Azimio la 2030 linahusisha ustawishaji wa viwanda na vituo vya mikakati ili kuongeza nafasi za kazi kwa mamia ya maelfu ya raia wa Saudia.

Maelezo zaidi na Labaan Shabaan