Kimataifa

Saudia yamnyonga yaya aliyemuua bosi aliyejaribu kumbaka

November 1st, 2018 2 min read

MASHIRIKA na PETER MBURU

SAUDI Arabia Jumatatu ilimnyonga mwanamke kutoka Indonesia ambaye alipatikana na hatia ya kumuua mwajiri wake 2011, hata bila kuiarifu serikali ya Indonesia.

Tuti Tursilawati ambaye alikuwa yaya alihukumiwa kifo na mahakama ya Saudi mnamo 2011, kwa kumuua mwajiri wake nchini humo. Bi Tursilawati alieleza korti kuwa alikuwa akijikinga baada ya bosi huyo kumvamia akitaka kumbaka.

Hatua hiyo sasa imezua tumbo joto baina ya uhusiano wa mataifa hayo mawili, kwani kulingana na sheria ya Indonesia, kabla ya hatua kama hiyo kuchukuliwa, wizara ya masuala ya nje huhusishwa.

Kutekelezwa kwa mauaji hayo ya Jumatatu katika Jiji la Thaif sasa kulifikisha mara nne kwa Saudi kutekeleza mauaji sawia kwa raia wa Indonesia ambao wanafanya kazi humo bila kufahamisha serikali hiyo, ndani ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Hadi sasa, kuna raia 18 wa Indonesia katika jela za Saudi ambao wamehukumiwa kifo.

Vilevile, kisa hicho kimetokea wakati serikali ya Saudi inasukumwa na jamii za kimataifa kuelezea kuhusu mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi.

Mwanamke aliyeuawa alieleza korti kuwa mwajiri wake alikuwa akimdhulumu kimapenzi na hivyo alikuwa akijitetea.

Vilevile, kuuawa kwake kulikuja wiki moja tu baada ya waziri wa masuala ya nje Saudi Arabia Adel al-Juber kukutana na mwenzake wa Indonesia na Rais Joko Widodo Jakarta, kuzungumzia masuala masuala ya haki za wafanyakazi wa mataifa hayo mawili.

Wakati wa mkutano huo, waziri wa masuala ya nje Indonesia Retno Marsudi alisisitiza kuwe na sheria ya lazima serikali yake iwe ikifahamishwa kabla ya hukumu za kifo kutekelezwa dhidi ya raia wake.

Serikali ya Indonesia aidha ilitaka uchunguzi wa kina ufanywe dhidi ya mauaji ya Khashoddi, ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Saudi.

Saudi Arabia ndilo taifa lililoajiri wafanyakazi wengi zaidi wa nyumbani kutoka Indonesiua duniani, na awali mwezi huu nchi hizo mbili zilielewana kufanya usimamizi wa pamoja kwa wafanyakazi hao.

“Ni wazi kuwa Saudi Arabia haitii makubaliano yaliyowekwa kuhusu kulindwa kwa wafanyakazi wa nyumbani, haswa kwa kutekeleza mauaji hayo,” akasema Wahyu Susilo, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kutetea maslahi ya wafanyakazi wa nyumbani kutoka Indonesia, huko Saudi.

Afisa huyo amemtaka rais wa nchi yake kuchukua hatua kali za kidiplomasia ili kuhakikisha kuwa tukio la aina hiyo halijirudii tena.

Serikali ya Indonesia, hata hivyo, ilikuwa imekata rufaa dhidi ya hukumu ya mwanamke huyo kortini na kwa mfalme wa Saudi, lakini serikali ya Saudi ikaendelea kutekeleza mauaji hayo.