SAUTI YA MKEREKETWA: Ada inayotozwa na KICD ili kuidhinisha vitabu yatisha kweli

SAUTI YA MKEREKETWA: Ada inayotozwa na KICD ili kuidhinisha vitabu yatisha kweli

Na HENRY INDINDI

MOJA katika masuala yanayozungumziwa kwa sauti za chini sana na wachapishaji na baadhi ya waandishi waliokuwa na nia ya kuwasilisha miswada au vitabu vyao kwa ajili ya kutathminiwa na Taasisi ya Ukuzaji Mitaala nchini (KICD), ni ada iliyowekwa kwenye mchakato huu.

Yamkini, ada iliyowekwa ni shilingi laki moja na elfu arobaini (140,000) kwa tathmini ya kwanza ya muswada na nyongeza ya laki moja (100,000) kwa uwasilishaji wa baada ya kushughulikia masahihisho. Hii ndiyo ada itakayotozwa kila muswada utakaowasilishwa KICD kwa ajili ya kutathminiwa na kuidhinishwa.

Ada hii itayahitaji mashirika ya uchapishaji kuwasilisha miswada na vitabu bora pekee badala ya kuwasilisha miswada mingine ya kubahatisha. Yaani hakuna shirika litakalojihimu kuwasilisha muswada ambao utatokomeza takribani shilingi laki tatu bila uhakika wa muswada kushindana kisawasawa. Isitoshe, miswada itawasilishwa michache kwa hivyo pana uwezekano macho ya watakaoshughulikia tathmini yatazamia uhakika wa kupata vitabu bora na fasihi bora.

Kwaza juhudi

Kwa upande wa pili, ada hii imekwaza juhudi za watu wengi. Katika shindano ambalo huna uhakika kuhusu kitu mahususi kinachoweza kukupa ushindi, ni vyema ukizitoa zana zako zote ili moja itakayofuma cha kukufaa ikufae.

Kwa kuweka ada kubwa kama hii, taasisi ya ukuzaji mitaala imewanyima wachapishaji mwao wa kutumia zana zao zote kufuma uidhinishwaji wa vitabu vyao. Na udhibiti wa aina hii unaweza kuwa na athari hasi kuliko unavyoweza kuwa chanya maanake katika ufinyu na uhaba wa mawazo yatakayowasilishwa, huenda mawazo yatakayoingia katika ulimwengu wa wanafunzi pia yakawa na uhaba na ufinyu huo.

Aidha, udhibiti wa ada hii unawanyima waandishi wa kujichapishia na mashirika yanayoibukia katika tasnia ya uchapishaji mwao wa kushiriki kwenye meza hii ya tathmini ya vitabu. Kuna waandishi ambao wamejichapishia mawazo mazuri sana.

Kwa hakika ukisoma baadhi ya vitabu vyao, unahisi kwamba vingestahili kutahiniwa katika mitaala yetu kutokana na mafunzo yaliyomo. Kwa kuwa waandishi na wachapishaji hawa chipukizi hawana mtaji wa kutosha kushiriki katika kinyang’anyiro ambacho masharti yake yamekuwa ghali sana, wanafunzi wetu watanyimwa fursa ya kukutana na mawazo haya bora.

Mawanda

Katika taifa hili tumeahidiwa mara kwa mara, wajasiriamali chipukizi watapata nafasi ya kushiriki biashara ili kupanua mawanda ya biashara na kuwaajiri watu wengi. Tunapoweka ada ghali kama hizi zinazowanyima wachapishaji chipukizi na waandishi wa kujichapishia mwao wa kushiriki katika mazingira yenye usawa na yanayowawezesha, bila shaka hatutakuwa na tunaafikia azimio hilo la kupanua biashara.

Huenda uamuzi wa kuweka ada hii kuwa juu unatokana na ukweli kwamba serikali imewamba, ama ina uchechefu wa pesa lakini hiyo hiyo serikali haiwezi kuwatarajia wachapishaji na wajasiriamali chipukizi kuwa na pesa ikiwa yenyewe haina. Biashara ya vitabu ilitikiswa pakubwa sana na korona, si haki kuiumiza hata zaidi kwa kuweka ada za kutisha.

You can share this post!

NASAHA: Nukta muhimu za kuzingatia mitihani ya kitaifa...

Nkana FC anayochezea Mkenya Abuya yaendea muujiza dhidi ya...