SAUTI YA MKEREKETWA: Heko wadau kuwezesha wapenzi wote wa Kiswahili kumwomboleza Walibora

SAUTI YA MKEREKETWA: Heko wadau kuwezesha wapenzi wote wa Kiswahili kumwomboleza Walibora

 

Na HENRY INDINDI

SASA tunakubali kwamba ndugu yetu Prof Ken Walibora alituacha maanake hatuna budi tena kukubali baada ya kushuhudia mazishi yake.

Tunachoweza kufanya kwa sasa ni kuiombea roho yake huko alikopumzishwa na kuiombea familia yake ijaliwe nguvu na uwezo wa kustahimili msiba.

Aidha, tutaendelea kupalilia matumaini na kushinikiza vyombo vya dola kushughulikia uchunguzi wa kilichosababisha kifo chake. Tunatamani kuona watu wakiwajibishwa kutokana na kutowajibika kwao katika kuyanusuru maisha ya Prof Ken Walibora. Ikiwa ni udhibiti wa sera katika hospitali ambazo huthamini majina ya watu na pesa zao badala ya maisha na uhai wao, tunataka kuona zikibadilishwa.

Pamoja na hayo tutaendelea kujifuta machozi na sasa tusherehekee maisha yake; kutangamana kwetu naye na mchango aali alioutoa kwa uhai na hadhi ya Kiswahili katika uzima wake. Ni hili linalonipa ujasiri wa kuwashukuru watu mahususi na makundi mbalimbali kwa kutuwezesha kuipokea michango hiyo na kumwomboleza kikamilifu. Safari ambayo imetuishia kuomba kwamba hiyo barabara iliyosababisha kifo chake, kwenye barabara ya Landhies ibadilishwe jina na kuitwa Barabara ya Ken Walibora.

Asasi mbalimbali zilizotupa nafasi ya kumwomboleza Prof Ken Walibora zimetusaidia sana kukikubali kifo chake. ‘Taifa Leo’, Redio Maisha, KBC Idhaa ya Taifa na Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) ni vyombo ambavyo vilitoa nafasi ya kisawasawa kwa wapenzi na walezi wa Kiswahili kumwomboleza mkota huyu wa fasihi ya Kiswahili.

Taifa Leo

Isitoshe, kwa niaba ya wengine nchini ninashukuru gazeti la ‘Taifa Leo’ kwa kutupa fursa ya kupata ‘Kina cha Fikra’ iliyotulisha ‘Kauli ya Walibora’ kila wiki. Haya yalitupa nafasi ya kupata mkondo wa fikira zake, msimamo wake na ukereketwa wake kwa lugha ya Kiswahili.

Ninatoa shukrani nyingine za kipekee kwa ndugu Simon Sossion, Mkurugenzi wa Shirika la Uchapishaji la Spotlight kwa kukitambua kipaji cha Ken Walibora na kumchapishia kazi zake. Ujasiri wa kumchapishia riwaya ya ‘Siku Njema’ akiwa Longhorn hatimaye uliizalia tasnia ya Kiswahili mwandishi aali ambaye ameacha alama kubwa katika maisha na uhai wa Kiswahili. Ndiye alikitambua kipaji changu cha kuandika na kunichapishia kazi zangu pia.

Huku kutambua vipaji ambavyo havikujulikana kabisa, kuvilea na kuviweka katika ramani ya ulimwengu kunapaswa kuigwa na wachapishaji wengine ambao walipofushwa awali na uchapishaji wa majina tajika katika jamii.

Naomba nitumie nafasi hii pia kuwahimiza waandishi chipukizi kuhakikisha kwamba wanaukuza ubunifu wao ili kuwaandikia wasomaji kazi zitakazoacha alama ya kudumu. Kila mara tujiulize kwamba na sisi itakapokuja nafasi yetu ya kuuondokea ulimwengu, tutakuwa tumeacha mchango gani wa kuuelekeza ulimwengu.

You can share this post!

Mji wa Thika wasafishwa na kunyunyizwa kuepuka Covid-19

Sonko amenyana na serikali

adminleo