SAUTI YA MKEREKETWA: Pendekezo la TSC kuifanyia mabadiliko kozi ya ualimu ni aula

SAUTI YA MKEREKETWA: Pendekezo la TSC kuifanyia mabadiliko kozi ya ualimu ni aula

Na HENRY INDINDI

WIKI iliyopita kulikuwa na taarifa kutoka kwa Tume ya Huduma za Walimu (TSC) kuhusu mabadiliko yanayopendekezwa kwenye kozi ya ualimu.

Yamkini kutakuwa na kituo au kitivo mahususi cha ufundishaji wa kozi za ualimu na miaka minne ya kwanza itumiwe katika kuzamia masomo watakayofundisha walimu hao.

Yaani pendekezo hili litaweka shahada ya ualimu katika ngazi na mkondo sawa na ule wa taaluma ya uanasheria. Mwalimu mtarajiwa atasomea masomo anayokusudia kufunza kwanza, ayazamie kisha ajiunge na chuo cha ualimu kwa mwaka mmoja kabla ya kufuzu kuwa mwalimu.

Pamoja na kuunga mkono pendekezo hili, kuna mambo ambayo itakuwa muhimu kuyaweka wazi. Kwanza ni madai kwamba walimu watarajiwa watasomea masomo matatu au kozi tatu kwa ajili ya masomo watakayofundisha nyanjani. Hili halina mashiko yoyote.

Ikiwa moja katika sababu za kupendekeza mabadiliko huenda ikatokana na hali kwamba awali walimu hawakuandaliwa kisawasawa katika masomo hayo waliyokusudiwa kufunza, basi nyongeza ya somo la tatu haibadili chochote. Wabaki na masomo hayo mawili ya awali na ujifunzaji wa masomo hayo uzamiwe kwa mazingatio ya maendeleo ya taaluma hizo.

Kumpa mwalimu mmoja masomo matatu ya kufundisha ni kuongeza mzigo katika maandalizi yake na bila shaka hatajiandaa vya kutosha kwa manufaa ya wanafunzi wake.

Kufundisha kunahitaji utafiti. Watapata wapi muda wa kutafitia masomo hayo matatu ili wabobee na kuwafundisha wanafunzi kwa dhati na kina? Ni afadhali wabaki na masomo mawili kisha wenyewe wateue masomo wanayotaka kubobea kwayo na kuzama zaidi ili ikiwezekana wafanye kozi nyingi za somo hilo chuoni.

Changamoto

Pili, walimu ambao sasa wanahudumu nyanjani na ambao tunaamini kwamba waliandaliwa vyema kabla ya kuajiriwa kufunza, watahitajika kuenda mafunzoni tena kupata stashahada ya ualimu? Ikiwa hatutawarudisha vyuoni kusomea ualimu tutachukua hatua zipi ili kuhakikisha kwamba wanakuwa katika upeo mmoja na wenzao watakaotoka vyuoni na mkondo huu mpya kuisomea taaluma? Labda haya pia yanahitaji ufafanuzi zaidi ili tuone iwapo walimu waliofuzu awali wataandaliwa kuweza kufundisha mtaala huu mpya wa umilisi na utendaji.

Isitoshe, huenda katika somo la Kiswahili huu ukawa wakati mwafaka wa kutenganisha isimu na fasihi. Badala ya kuzisomea zote pamoja kama Kiswahili, Isimu na lugha liwe somo tofauti na fasihi ilivyo katika Kiingereza.

Kwa kufanya hivi, wanagenzi au walimu watarajiwa vyuoni watapata muda wa kusoma vitabu vingi vya fasihi na kujiandaa vyema katika ufundishaji wa vitabu hivyo au vitabu vingine vya fasihi.

Kusoma vitabu vingi vya waandishi mbalimbali kutawasaidia walimu hawa watarajiwa kutagusana na mitindo na mikondo mbalimbali ya kuyaeleza mambo. Aidha, hili litachochea mabadiliko katika mikondo na masuala yanayoandikiwa na waandishi ili kutanua wigo wa maudhui katika fasihi ya Kiswahili.

Mabadiliko ni kitu aushi na yapo yanayokuja na heri. Tunapoliunga mkono pendekezo hili, meza ya Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC), iangalie mbinu bora zaidi za kutekeleza wazo hili.

You can share this post!

KINA CHA FIKRA: Mafanikio na mazonge tangu tupate madaraka

Ugumu wa maisha tangu makazi kadhaa yabomolewe eneo la Njiru