SAUTI YA MKEREKETWA: Pumzika kwa amani Jemedari Magufuli

SAUTI YA MKEREKETWA: Pumzika kwa amani Jemedari Magufuli

Na HENRY INDINDI

KESHO kutwa katika mkoa wa Geita, eneo la Chato, nchini Tanzania kunafukiwa balozi na mtetezi mkubwa wa Kiswahili Afrika Mashariki.

Kusema la kweli huku ndugu zetu wa Tanzania wakiomboleza kwa kupoteza jembe la kuchapa kazi, sisi umma wa Kiswahili tunalilia kumpoteza balozi mkubwa sana wa Kiswahili.

Ninafurahi na kushukuru Mungu kwamba mimi na ndugu yangu Mwl. Andrew Watuha wa Chuo Kikuu cha Nairobi, tulishiriki kongamano la kumtuza na kumuenzi Rais Magufuli mjini Dodoma mapema mwaka 2021 kwa juhudi zake za kupigania na kueneza Kiswahili ulimwenguni.

Hayati Rais Pombe Magufuli hakufungua milango ya Kiswahili kwa kuongoza uundaji wa sera za kunyanyua Kiswahili nchini Tanzania tu. Ndiye aliyewatangazia na kuwaumbua wenzake wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu haja ya kutumiwa kwa Kiswahili katika shughuli zote za Jumuiya.

Hakuelewa ni vipi kanda hii ya Afrika Mashariki iliyo na lugha yake ya kuiunganisha ambayo tunaweza kuitaja kama lingua franka yake, inaweza kuendelea kuishi katika vivuli vya wakoloni na kukazania kutumia lugha za wakoloni. Haikumwelea vizuri kwamba shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki, zitafanyika katika lugha za kigeni huku kukiwa na Kiswahili ambacho kina uwezo wa kila kitu.

Kutokana na juhudi hizi, tulianza kuona mabadiliko ingawa yakiingia kwa mwanga hafifu kutokana na mazoea ya baadhi ya mataifa ya ukanda huu. Yapo mataifa ambayo yanaamini kwamba huenda yakiacha kuishi katika vivuli vya wakoloni yataugua maradhi mabaya na hatari sana kushinda korona na ebola. Huku kujikokota kwa baadhi ya wenzake katika jumuiya, kulimshawishi kuachana nao. Akafanya safari za mataifa ya Kusini mwa Afrika, akiwapelekea wenyeji wake vitabu, kamusi na wataalamu wa Kiswahili. Hili lilizaa matunda, Afrika Kusini wakaingiza ufundishwaji na ujifunzaji wa Kiswahili katika mtaala wao.

Kwake nchini Tanzania, ameacha sera za kunyanyua Kiswahili zikitononoka kwelikweli. Alipoziuliza mahakama kuhusu sababu zao za kutoa maamuzi ya kesi katika Kiingereza na ikiwa hilo kweli lilikuwa na mafao kwa wananchi wote Tanzania hadi vijijini, tumeona mabadiliko katika mfumo wa lugha ya mahakama. Sasa ni rasmi Tanzania inajitahidi kuweka maamuzi ya mahakama katika Kiswahili. Aidha, ofisi zote za balozi zao katika mataifa ya kigeni, zitakuwa na meza pamoja na chuo japo kidogo cha kufundisha Kiswahili kwa wageni. Haya ndiyo mawazo ambayo baadhi yetu, tumejaribu kulipa taifa letu kwa muda mrefu lakini, huku kwetu tunakuwa mashujaa wa kusema tu.

Kwa kuondoka Jembe, WaTanzania wamepoteza, Jumuiya ya Afrika Mashariki imepoteza na sisi katika Kiswahili tumepoteza hata zaidi. Tunahitaji mabalozi kama yeye ili Kiswahili kiwe chumo la ajira kwa wengi ulimwenguni. Tunahitaji viongozi jasiri kama yeye ili kinachotoka Afrika kionekane kuwa na thamani machoni mwa ulimwengu. Tunahitaji viongozi wazalendo wa kisawasawa kama yeye, ili kujua kwamba amali na vito vya kutoka Afrika Mashariki vinaweza kupokelewa na kufurahiwa ulimwenguni. Pumzika kwa amani Jemedari Pombe Magufuli.

You can share this post!

KAULI YA MATUNDURA: Mshabaha kati ya Rais Magufuli na...

USWAHILINI: Mnara wa pembe jijini Mombasa ndio nembo kuu ya...