SAUTI YA MKEREKETWA: Sekta ya elimu nchini itafaidi iwapo walimu watakubali mafunzo

SAUTI YA MKEREKETWA: Sekta ya elimu nchini itafaidi iwapo walimu watakubali mafunzo

Na HENRY INDINDI

MJADALA umekuwepo nchini kuhusu mafunzo ya kisarifu kwa walimu ilivyopendekezwa na mwajiri wao, Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC).

Mwanzoni walipoitangaza nia ya kutekeleza mafunzo haya asilimia kubwa ya walimu walilalamikia hilo na kuahidi kutoshiriki.

Kilio chao kilikuwa kwenye ada za mafunzo, haja ya mafunzo yenyewe na vyuo vikuu vilivyoteuliwa kuyatekeleza. Kusema la kweli, wengi hawakujua mwanzoni kwamba hayo yaliyotangazwa yalikuwa katika sheria ya TSC.

Waliikemea Tume kwa kufanya uamuzi bila kushauriana na walimu kupitia kwa vyama vyao na kufikia sasa ni dhahiri kwamba walimu wanapinga wazo hilo.

Tutangulize kwa kusema hapa kwamba mafunzo ya kujiimarisha na kujisarifu ni muhimu hasa ikichukuliwa kwamba ulimwengu unabadilika kila uchao na mahitaji na matarajio yake vilevile.

Kwa maana hii, kila mwanataaluma katika taaluma yake anahitajika kufanya kozi mbalimbali muda baada ya muda ili aweze kuenda na uchao katika taaluma husika.

Hadharauliwi mwanataaluma yeyote anapokumbushwa kuhusu haja ya kujinoa hata zaidi ili aifae taaluma vyema zaidi katika umbo la mabadiliko yake.

Teknolojia hivi sasa ni sehemu ya maisha na ni hakika kwamba baadhi ya walimu wanahitaji kunolewa upya katika masuala haya ya teknolojia na jinsi tunavyoweza kuitumikisha kazini.

Fursa zinapopatikana kama hizi za mafunzo ya kujinoa, tuzichangamkie kama njia ya kudhihirisha kwamba tunataka kuenda na uchao katika taaluma yetu.

Isitoshe, tumeingia katika mtaala mpya wa elimu, CBC, unaowahitaji walimu kuelekezwa hata zaidi kuhusu jinsi ya kuufanikisha.

Malalamishi tuliyokuwa nayo baadhi yetu kwamba hatukuwa tumefunzwa vyema kuuwezesha mtaala huu mpya, yatashughulikiwa kwa kukubali kupokea mafunzo haya ya kisarifu.

Changamoto

Ila ninayoiona mimi itakuwa katika mchakato wa kulitekeleza hili la mafunzo.

Inawezekana litatikisa baadhi ya asasi za jamii kama ndoa hasa iwapo wanandoa hao wote ni walimu na wameenda kwa mafunzo pande mbalimbali.

Pili, ingekuwa vyema zaidi ikiwa tume ingejihimu kufanyia walimu tathmini ili kutambua udhaifu wao.

Huenda kuna walimu wanaohitaji kunyanyuliwa katika mbinu za kufundishia masomo yao pekee na pakawa na wengine ambao huenda mahitaji yao yakawa katika masomo mahususi wanayofundisha.

Tume haifai kuchukulia kwamba udhaifu na mahitaji ya walimu wote ni sawa na hivyo kuwasukumizia kila kitu katika mafunzo. Hapo hawatakuwa wamewafaa walimu.

Kuhusu vyuo vikuu vilivyoteuliwa, kuna haja ya kushauriana zaidi kuhusu ikiwa inawezekana walimu wakayapate mafunzo hayo katika vyuo vikuu vilivyo karibu nao.

Kingeteuliwa angalau chuo kikuu kimoja katika kila eneo (katika mikoa ya zamani) ili walimu wanaotoka katika mkoa huo wayapate mafunzo yao huko.

Aidha, kwa kuwa vyuo vikuu vya umma vimekuwa na kilio kuhusu uhaba wa pesa, labda hii ingekuwa mojawapo katika fursa za kuviwezesha kupata pesa.

Hata hivyo, ibainike kwamba katika Sheria hiyo ya TSC, tume ina mamlaka ya kuteua vyuo na haigizwi popote kushauriana na yeyote kulihusu suala hilo.

You can share this post!

NDIVYO SIVYO: Ukanushi wa kitenzi kishirikishi kipungufu...

KINA CHA FIKIRA: Ujeuri wa mpapai hujeruhi na udhalili wa...